Wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoka katika kata 21 za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao wanapotuumikia wananchi.
_
Mafunzo hayo yametolewa leo Jumatano Januari 08, 2025 katika ukumbi wa Dkt. Samia Katika Chuo Cha Ualimu Kasulu na wakufunzi kutoka Chuo Cha Serikali Za Mitaa (Hombolo) kilichopo mkoani Dodoma na kuhusisha makundi hayo.
_
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Dkt. Semistatus H. Mashimba amewataka washiriki hao kutambua nafasi zao kwa kuwa raia wema ikiwemo kuongoza kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.
_
“Nafasi zenu ni kubwa lakini msivae hizo nafasi zenu mkawe wananchi wema kwani mkifanya hivyo mtawatumikia wananchi kwa uadilifu...msiende mkawa miungu watu mkawe wasikivu kwa wananchi na mkafate misingi ya uongozi na utawala bora,”amesema Dkt. Mashimba.
_
Katika hatua nyingine Dkt. Mashimba amewataka washiriki hao kufanya tathmini ya mara kwa mara ya utendaji wao wa kazi ikiwemo kutokufanya vitu kinyume na utaratibu kwa kufanya vikao vya kisheria pamoja na kuhakikisha wanasoma taarifa ya mapato na matumizi kwa wananchi.
_
Naye Mhadhiri wa Chuo cha Hombolo,Sarah Kilagane ameyataka makundi hayo kusimama vizuri kwenye nafasi zao kwa kazi kwa ushirikiano mkubwa na wananchi ili kuwaletea maendeleo.
_
"Swala la uibuaji na usimamiaji wa miradi na vyanzo vya mapato ni swala muhimu la kuzingatia katika kutekeleza majukumu yenu likiwemo jukumu kubwa la kusimamia masuala ya ulinzi na usalama wa kijiji husika...sifa za kiongozi bora ni mtu kuwa muadilifu na mfano wa kuigwa kwenye jamii,ambaye anashirikiana na wananchi kwenye kuleta maendeleo na anayesimamia mawasiliano kutoka ngazi za chini kuyaleta juu," ameongeza.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.