Na Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma leo Jumamosi Oktoba 18, 2025, imefanya tukio la kihistoria kwa kukabidhi basi jipya la kisasa lenye thamani ya Shilingi milioni 160 kwa shule ya Hope Pre and Primary, yenye mchepuo wa Kiingereza, kwa ajili ya kubebea wanafunzi. Basi hilo limenunuliwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amempongeza Mkurugenzi kwa jitihada zake za kuboresha miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa bweni na ununuzi wa gari jipya. Amesema hatua hizo zitavutia wazazi kutoka sehemu mbalimbali kuwaleta watoto wao shuleni hapo.
“Shule hii inatakiwa kuwa kubwa na ya mfano kwani ndiyo ya kwanza mkoani kufundisha mchepuo wa Kiingereza. Namwelekeza Mwalimu Mkuu kuhakikisha miundombinu iliyopo inatunzwa vizuri, na yule atakayepatiwa dhamana ya kuendesha gari hili ahakikishe anabeba wanafunzi kwa usalama,” amesema Kanali Mwakisu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, CPA Francis Kafuku, amemshukuru Rais kwa kuridhia matumizi ya fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kuboresha miundombinu ya shule hiyo, ikijumuisha bweni na ununuzi wa gari, hatua ambayo itasaidia ubora wa ujifunzaji na ufundishaji.
“Mahitaji yote yanatokana na mapendekezo ya madiwani, ambayo halmashauri inampelekea Mkuu wa Wilaya kubariki. Tunamshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kubariki mambo haya, kwani angeweza kukataa fedha hizo ziende kwa miradi mingine,” amesema CPA Kafuku.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Awali naMsingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, amesema kuwa kutokana na muitikio mkubwa wa wazazi kuleta watoto shuleni hapo, kulikuwa na changamoto ya usafiri.Hivyo basi hilo jipya litasaidia kupunguza adha hiyo kwa wanafunzi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.