Na Mwandishi Wetu
Taasisi isiyo ya kiserikali ya LALJI Foundation imetoa msaada wa madawati 100 kwa shule za msingi Chekenya, Katoto na Nyakasanda wilayani Kasulu, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo Jumamosi, Oktoba 4, 2025, katika Shule ya Msingi Chekenya, Kata ya Kurugongo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema msaada huo utasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora zaidi, jambo litakalopunguza utoro na kuongeza ufaulu.
“Utoaji wa madawati haya unaonyesha namna ambavyo Serikali ina ushirikiano mzuri na wadau wa maendeleo. Kupitia taasisi kama hizi, tunaweza kushirikiana kutekeleza yale ambayo Serikali haiwezi kuyafanya mara moja. Ndiyo maana tunahamasisha uwekezaji unaogusa jamii ili kuchochea maendeleo,” amesema Kanali Mwakisu.
Ameongeza kuwa, ni jukumu la wanafunzi waliopata msaada huo kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao na kuwa viongozi bora wa baadaye katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake, Mlezi wa taasisi hiyo, Sheni Lalji, amesema utoaji wa madawati hayo unalenga kujenga mazingira bora ya kujifunzia yenye heshima, kuboresha upangaji wa madarasa, kuongeza ufanisi wa walimu, kupunguza utoro na kusaidia Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chekenya, Benjamini Mwapule, ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo, akibainisha kuwa madawati 25 waliyopokea yatasaidia zaidi ya wanafunzi 100 kukaa kwa utulivu na kujifunza katika mazingira bora.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.