Na Mwandishi Wetu
Maafisa ugani wametakiwa kuhakikisha wakulima wanasajiliwa kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea ili waweze kunufaika na punguzo la bei ya mbegu na mbolea katika msimu mpya wa kilimo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mikidadi Mbaruku, ametoa agizo hilo leo wakati akifungua kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa watendaji wa divisheni hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Kagoma, makao makuu ya Halmashauri.
“Nataka mhakikishe wakulima wanasajiliwa kwenye mfumo huo ili wapate punguzo la mbegu na mbolea kwa kutumia namba zao hizo hizo. Pia, tembeleeni wakulima kipindi hiki wanapoandaa mashamba kuwaelimisha kuhusu uchaguzi wa mbegu bora, upandaji kwa nafasi sahihi na matumizi sahihi ya pembejeo,” amesema Mbaruku.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali Watu wa Halmashauri hiyo, Phebby Ambwene, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia muda katika utekelezaji wa majukumu yao ili kazi zikamilike kwa wakati uliopangwa.
Aidha, amewasisitiza kuepuka migogoro hasa ya ardhi, na pale inaposhindikana kutatuliwa katika ngazi za chini, wahakikishe inafikishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi kwa hatua zaidi.
Katika hatua nyingine, Afisa Umwagiliaji wa Halmashauri hiyo, Rajab Kisigalile, ameipongeza Divisheni ya Kilimo kwa kuandaa kikao hicho, akisema kimekuwa fursa muhimu kwa wataalam kukumbushwa majukumu yao na misingi ya utumishi wa umma.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.