Na Mwandishi Wetu
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Wakili Emmanuel Ladislaus, amewataka wasimamizi wa vituo na wasaidizi wao kuhakikisha wanafika mapema vituoni na kukamilisha maandalizi yote kabla ya saa 1:00 asubuhi ili wananchi waanze kupiga kura kwa wakati.

Wakili Ladislaus ametoa maelekezo hayo leo Jumapili, Oktoba 26, 2025, katika Chuo cha Ualimu Kasulu (TCC) wakati akifungua Semina ya Uchaguzi kwa wasimamizi wa vituo na wasaidizi wao.

Amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema akisema ni jambo lisilokubalika kuanza kuandaa kituo wakati muda wa kupiga kura ukiwa umeshawadia.

“Kwakweli itakuwa jambo la ajabu sana inapofika saa 1:00 asubuhi wewe ndio unaanza kuandaa kituo. Maandalizi hayo yanatakiwa kufanyika mapema ili inapofika muda huo watu waanze kupiga kura baada ya maandalizi yote kukamilika,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwapa kipaumbele wapiga kura wenye mahitaji maalum, wakiwemo wajawazito, wazee wenye umri kuanzia miaka 60, walemavu na akinamama wanaonyonyesha, akibainisha kuwa kundi hilo linapaswa kutangulizwa kupiga kura.

“Tunaposema mahitaji maalum ina maana pana. Niwaombe watu wa aina hii muwape nafasi za mwanzo wanapofika kituoni,” ameongeza.

Kadhalika, Wakili Ladislaus amewataka wasimamizi wa vituo kuhakikisha wanafanya mawasiliano ya karibu na wasimamizi wasaidizi wa kata ili kushirikiana katika kutoa ufafanuzi na kutatua changamoto zitakazojitokeza, kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika kwa utulivu na ufanisi katika maeneo yote waliyopewa dhamana.

HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.