Na Mwandishi Wetu
Wazazi na wanafunzi walioudhuria Mahafali ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Nkundutsi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuwa mabalozi katika kuhamasisha umma kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura zoezi linalotarajiwa kuanza Oktoba 11, 2024 na kufikia tamati mnamo Oktoba 20,2024.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele leo Alhamisi Oktoba 3,2024 alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo na kubainisha kuwa kwa kufanya hivyo itasaidia kupata viongozi sahihi wa Serikali za Mitaa wenye kubeba dhamana ya maendeleo katika maeneo yao.
“Tukiwa tunaelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 maandalizi yameiva ninahamasisha wananchi wote mliopo hapa na wahitimu mliofikisha umri wa miaka 18 muende mkajiorodheshe kwenye daftari la kupiga kura tupate viongozi watakaoharakisha maendeleo yetu kwa mustakabali mzima wa taifa letu,” amesema.
Aidha, Theresia amewataka wanafunzi wanaondelea na masomo katika shule hiyo kutia bidii katika masomo baada ya wenzao kuhitimu ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka kitu kitakachosaidia jina la shule hiyo kupaa maeneo tofauti hapa nchini.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Focus Albert amehimiza wazazi ambao watoto wao watachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza hapo mwakani kuhakikisha wanaripoti mashuleni na kuwafuatilia mwenendo wao ili waweze kumaliza hadi kidato cha nne.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Dunstan Munyungu matarajio yao ni kufuta matokeo ya sifuri na kupunguza daraja la nne na mikakati tayari imewekwa katika kufanikisha hilo ndio maana wamekuwa shule ya kwanza kwenye mitihani ya kujipima kwa ngazi ya halmshauri.
Katika mahafali hayo ilishuhudiwa iadadi ya wahitimu 95 ambapo wavulana ni 45 na wasichana ni 50.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.