Wanafunzi washiriki wa Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wametakiwa kuwa na nidhamu na kujituma muda wote wawapo kambini ili waweze kupata matokeo mazuri kwenye michezo hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Semistatus H. Mashimba wilayani humo leo Jumamosi Juni 1,2024 alipokua anafungua mashindano hayo na kuwataka wasishiriki mashindano husika kwa mazoea bali wafanye mbinu ili kuibuka na ushindi.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia washiriki hao kuweza kushinda katika mashindano ya UMISETA kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa na kuwaahidi kuwa iwapo watafanikiwa kufanya hivyo ataipa kipaumbele sekta ya michezo katika halmashauri anayoiongoza.
Aidha, Dkt. Mashimba amewataka watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha afya na usalama wa wanamichezo unakua vyema wakati wote wawapo kambini kuanzia siku ya ufunguzi hadi kambi yao itakapovyunjwa.
"Nitoe shime kwa Afisa Mtendaji wa Kata na Kijiji tuhakikishe walimu na watoto hawa wako salama na mawasiliano yanakuwepo ili tuhakikishe tunaanza na kumaliza mashindano yetu salama", amesema.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo, Iyogo Isuja amesema uwepo wa UMISETA mashuleni si upotezaji wa muda ila inawapa nafasi nzuri wanafunzi ambao ni washiriki wa michezo hiyo kuweza kufanya vizuri katika masomo pia.
Ambapo ameongeza kuwa kwa kushiriki michezo hiyo inawapa nafasi nzuri washiriki kujenga afya na akili zao kuwa vizuri pamoja na kuwa na fursa nzuri katika soko la ajira nchini.
Kwa upande wake Afisa Michezo wa Halmashauri hiyo, Thomas Kisaka amesema matumaini ni makubwa ya kushinda michezo hiyo kwa ngazi zote watakazoshiriki kutokana na maandalizi mazuri waliyotoa walimu wa michezo waliokuwa nao.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.