Na Mwandishi Wetu
Kufunguliwa kwa ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NRFA) wilayani Kasulu utatengeneza soko la uhakika la mazao utakaosaidia wakulima kujikomboa kiuchumi hivyo pato la kaya kuimarika.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele ameyabainisha hayo jana kwenye sherehe ya siku ya wakulima wa zao la Mpunga zilizofanyika katika Kijiji cha Titye wilayani humo.
“NRFA mwaka huu itaanza kununua mazao ikiwemo Mpunga tofauti na hapo awali soko lilipokuwa linaendeshwa na wafanyabiashara tulipokea malalamiko katika masuala ya vipimo hivyo NRFA itazingatia uaminifu wakulima wasiweze kuibiwa,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kuhimiza tafiti za mbegu bora zinazoweza kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Katika hatua nyingine Theresia amewapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kuunganisha nguvu na kutengeneza miundombinu ya madaraja ambapo ametoa ahadi ya kuwasiliana na Wakala wa Barabara Vijiji na Mjini (Tarura) kuifanyia maboresho.
Naye Mkurugenzi -TARI Kihinga, Dkt. Filson Kagimbo amesema mradi wa urutubishaji wa mazao (NUT-CAT) unafanyika katika nchi kumi barani Afrika kwenye mazao ya Ngano, Mahindi, Mpunga na Teff.
“Kwa hapa Tanzania mradi huu unafanyika katika Mkoa wa Kigoma kwenye wilaya tatu za Kakonko, Kasulu na Kigoma …hapa Kasulu Mahindi tunafanya katika kata za Nyenge, Rusesa na Kwaga huku kwa zao la Mpunga tunafanya katika Skimu ya Umwagiliaji ya Titye,” amesema.
Amesema kupitia tathimini waliyoifanya wamejiridhisha kuwa mavuno yameongezeka kutoka gunia tano hadi 12 ilivyokuwa awali na kufikia 25 mpaka 31 kwa heka moja.
Mhandisi wa Kilimo Mkoa wa Kigoma, Bathromeo Morice amesema kuwa kutokana na wakulima kufuata ushauri wa kitaalam umesaidia mkoa kupata zawadi ya uzalishaji wa mazao ya Mahindi na Mpunga katika sherehe za Nanenane za mwaka uliopita mkoani Mbeya.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Kasulu, Everine Reuben amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowawezesha wakulima wa sekta ya umwagiliaji.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.