Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Kikosi cha 825 Mtabila leo Jumatatu kimekabidhi madawati 250 na meza sita vyenye thamani ya shilingi 7,278,400 kwa Shule ya Msingi Mgombe, wilayani Kasulu. Hatua hiyo imepunguza changamoto ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo.
Aidha, kikosi hicho kimekarabati madawati 45 na hivyo kumaliza kabisa upungufu wa samani hizo, sambamba na kuwasaidia walimu saba kufundisha wanafunzi kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, kwa kuruhusu kambi hiyo kutekeleza jukumu hilo, jambo alilosema limeokoa zaidi ya shilingi milioni 13.
“Nimeambiwa thamani ya dawati moja ni shilingi 70,000, hivyo mmeokoa zaidi ya shilingi milioni 13 kama Mtabila wasingesaidia. Nawasihi jamii ya hapa muendelee kushirikiana na majirani zenu, mkikaa hapa mnakaa kama Watanzania. Shirikianeni ili kukuza ustawi wa nchi yetu,” amesema Kanali Mwakisu.
Aidha, amekiomba kikosi hicho, ambacho kina mikakati ya kuanzisha chuo cha ufundi wilayani humo, kitoe maombi ya eneo katika Kijiji cha Mgombe ili kutekeleza mpango huo, akisisitiza kuwa chuo hicho kitakuwa na tija katika kufundisha fani mbalimbali.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi hicho, Luteni Kanali Patrick Ndwenya, amewahimiza wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka kambi hiyo wasisite kuwasiliana nao wanapokumbana na changamoto mbalimbali, ili taratibu zifuatwe na msaada upatikane kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, ameishukuru kambi hiyo kwa msaada huo, akibainisha kuwa ofisi yake itahamasisha vijiji vingine kuiga mfano wa Shule ya Msingi Mgombe kwa kuwa wanufaika wakuu ni watoto.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.