Na Mwandishi Wetu
Serikali za Tanzania na Burundi leo, Jumamosi Agosti 16, 2025, zimeweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Mwendokasi (SGR) kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Musongati nchini Burundi, yenye urefu wa kilomita 300.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu dola bilioni 2.154 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 72, sawa na miaka sita.
Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika Musongati, Rais wa Burundi, Mhe. Évariste Ndayishimiye, ameishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo na usalama wa nchi hiyo.
Amesema ujenzi wa reli hiyo utakuwa kichocheo cha kiuchumi kwani utarahisisha usafirishaji wa malighafi kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea migodi ya Nikeli iliyoko Musongati, na kisha kusafirishwa kwenda masoko mbalimbali duniani.
“Nashukuru Tanzania kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo nchini kwetu. Tayari imetupatia bure sehemu ya Bandari Kavu Kigoma kwa ajili ya mizigo, na pia kiwanja eneo la Kwara, mkoani Pwani, kitakachotumika kujenga Bandari Kavu,” amesema Rais Ndayishimiye.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Umoja wa Afrika inayolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2063 bara lote linakuwa na mtandao bora wa miundombinu ya usafirishaji.
“Reli hii itafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wetu. Kwa mfano, safari ya kutoka Bujumbura hadi Dar es Salaam kwa sasa huchukua saa 96 kwa gari, lakini kupitia reli hii itapungua hadi saa 20 pekee. Hii itapunguza gharama za usafirishaji kwa zaidi ya 40%,” amesema Majaliwa.
Awali, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Mhe. Prof Makame Mbarawa, amebainisha kuwa reli hiyo itakapo kamilika itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani 3,800 za mizigo kwa wakati mmoja, hatua itakayopunguza gharama na ushuru wa bidhaa kati ya nchi hizo mbili jirani.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.