Na Mwandishi Wetu
Umoja wa Walimu na Wazazi (UWAWA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma umeanzisha mpango kabambe wa kushirikiana kuboresha elimu, ukiwaleta pamoja walimu na wazazi ili kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wa shule za sekondari, ikiwemo utoro, usalama na ustawi wa wanafunzi.
Akizungumza leo Jumatano Agosti 20, 2025 katika Chuo cha Ualimu Kasulu (TTC), Mratibu wa mafunzo hayo, Mwl. Pius Lijuwe, amesema hatua hiyo imelenga kuwajengea walimu na wazazi uelewa wa pamoja ili kusimamia kwa karibu maendeleo ya watoto wao na kuongeza ubora wa elimu wilayani humo.
Kwa upande wake, Diana Gwandu, ambaye ni mkufunzi wa mafunzo, ameeleza kuwa ushirikiano huo utaimarisha nidhamu na kuchochea ukuaji wa Idara ya Elimu Kasulu, huku wazazi na walimu wakishirikiana katika kila hatua ya safari ya kielimu ya watoto.
Walimu walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Mwl. Mussa Dede na Philipina Pius, wamesema mpango wa UWAWA utasaidia kudhibiti utoro, kukuza uhusiano wa karibu kati ya walimu na wanafunzi pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Aidha, mzazi Stela Mnenwa ameshukuru wadau wa elimu waliosaidia kufanikisha mafunzo hayo, akisisitiza kuwa hatua hiyo itawajengea wazazi uelewa wa kushirikiana zaidi na walimu kwa manufaa ya wanafunzi.
UWAWA ni mpango wa mafunzo ya ushirikiano kati ya walimu na wazazi unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania, Serikali ya Qatar na Shirika la UNICEF, ukiwa na lengo la kukuza sekta ya elimu nchini kwa kuweka msingi wa mshikamano wa jamii katika malezi na maendeleo ya wanafunzi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.