Na Mwandishi Wetu
Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Masumbuko Kwelema, amesema kuwa ugawaji wa bure wa miche ya kahawa aina ya Arabica umeleta matokeo chanya kwa kuongeza idadi ya wakulima kutoka 50 hadi kufikia 350 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea miradi ya kilimo katika Kata ya Buhoro, Kwelema amebainisha kuwa mbegu hiyo iliyoboreshwa imeonyesha mafanikio makubwa kutokana na uwezo wake wa kuzaa kwa wingi na kustahimili magonjwa.
“Awali, uzalishaji ulikuwa kati ya tani mbili hadi tatu kwa mwaka, lakini mwaka jana tulifikia tani 91.2 kutokana na hamasa na ugawaji wa miche bure. Mwaka huu tunatarajia kuvuna tani 120. Kupitia kitalu kipya cha Shule ya Msingi Kibilizi, tayari tumezalisha miche 384,000 kwa ajili ya kugawa kwa wakulima, na tunalenga kufikia miche 1,000,000,” amesema.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Buhoro, Stanslaus Petro, amesema kuwa kitalu na shamba la kahawa lililoanzishwa shuleni hapo limeiwezesha shule kupata fedha za kununua sukari kwa ajili ya uji wa wanafunzi, hatua iliyopunguza utoro na kuongeza ufanisi wa masomo.
Naye mkulima kutoka Kijiji cha Kibilizi, Lidia Kasmiri, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia miche pamoja na kuwapatia wataalam wa kilimo wanaotoa ushauri kuhusu upandaji, utunzaji na matumizi ya dawa, hali iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija shambani.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buhoro, Fredrick Nyamwombo, amesema kuwa kupitia mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na Serikali, wakazi wa kijiji hicho wamefanikiwa kuanzisha AMCOSS kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa zao hilo, jambo litakalosaidia kupunguza umaskini kijijini.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.