Na Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma leo, Jumatatu Septemba 15, 2025, imekabidhi rasmi Kituo cha Polisi cha Nyakitonto kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu. Kituo hicho chenye hadhi ya Daraja B, kimegharimu shilingi milioni 114 na kimejengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mwakisu ameipongeza Halmashauri kwa hatua hiyo akisisitiza kuwa kituo hicho kitatoa huduma za saa 24, jambo litakaloongeza ufanisi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi.
“Halmashauri hii ni mpya, na maendeleo hayawezi kufanikishwa bila usalama. Uwepo wa kituo hiki utakuwa chachu ya maendeleo mapya. Watu wataanza kuhamia, kujenga makazi na shughuli za kijamii na kiuchumi zitakua kwa kasi zaidi,” amesema.
Aidha, Mhe. Mwakisu ametumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wote waliopata nafasi ya kuongoza Halmashauri katika kipindi cha ujenzi wa kituo hicho, akiwataja Mkurugenzi wa kwanza Joseph Kashushura, aliyefuata Dkt. Semistatus Mashimba na Mkurugenzi wa sasa CPA Francis Kafuku.
Amesema mshikamano wa kiuongozi, dhamira ya pamoja na uwajibikaji wa viongozi hao ndio nguzo kuu iliyopelekea kukamilika kwa mradi huo, ambao utabaki kuwa alama ya mshikamano na kielelezo cha uwajibikaji kwa vizazi vijavyo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.