Na Mwandishi Wetu
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika Machi 8 kila mwaka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu leo Alhamisi Machi 6,2025 imefanya maadhimisho hayo kiwilaya katika Shule ya Sekondari Muyovozi.
Ambapo kupitia shughuli hiyo iligawa taulo za kike,katoni za vinywaji laini pamoja na kuendesha mijadala mbalimbali kuhusiana na namna ya kumkwamua mtoto wa kike kwa shule hiyo pamoja na wenzao wa Ntamya.
Akizungumza katika tukio hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu,Theresia Mtewele ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kuwa kwa zaidi ya miaka 30 inaposheherekewa siku hiyo kumekuwa na harakati mbalimbali za kumkomboa mwanamke zilizomsaidia kushika nafasi kubwa kwenye vyombo vikubwa vya kimaamuzi.
“Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake mwaka 2025 tunasheherekea mafanikio ambayo wanawake tumefikia katika nyanja mbalimbali kama uwakilishi kwenye uongozi na tunaye Rais ambaye ni mwanamke tunasheherekea vitu hivi tukiwa na mifano halisi ya wanawake ambao wameweza kuingia katika nafasi kubwa za kimaamuzi,” amesema.
Naye mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024, Makwaya Makwaya amesema kuwa Ili mtu aweze kufikia ndoto zake ni lazima azingatie suala la nidhamu na kujituma kwakuwa haitatokea mtu kukudhamini au kukupa nafasi usipozingatia mambo hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Victoria Makyao amesema kuwa madhamisho hayo huwa na lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake katika kufikia maendeleo kuona ni namna gani wanazipatia ufumbuzi.
Katika hatua nyingine Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Muyovozi,Joina Dismas amesema kuwa maadhimisho hayo yamemsaidia kujifunza wanawake ni watu kama watu wengine katika jamii hivyo wanatakiwa kuheshimiwa,kutunzwa pamoja na kuthaminiwa ili waweze kufikia ndoto zao.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.