Na Mwandishi Wetu,Kasulu
Wajumbe wa Kikao cha Mkataba wa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuhakikisha shughuli zote wanazozifanya zinatoa matokeo chanya kwa jamii kuelewa masuala ya lishe.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Novemba 23,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Dkt.Semistatus H.Mashimba wakati alipokuwa anaongoza mjadala kwenye kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kashushura uliopo katika makao makuu ya halmashauri hiyo.
"Niwaombe viongozi wa dini mtumie vipindi vyenu mnavyofanya mashuleni kuwashawishi suala la lishe wanafunzi ili waweze kufikisha ujumbe huo kwa wazazi wao ni vyakula gani vinafaa kukabiliana na tatizo la udumavu,uzito pungufu na ukondefu," amesema.
Aidha,Dkt.Mashimba amewataka wajumbe hao kushirikiana na wataalam wa lishe kubaini sehemu zilizoathirika zaidi na masuala ya udumavu,ukondefu na uzito pungufu na ikiwezekana watoe ushauri elekezi ni namna gani wanaweza kukabiliana na matatizo hayo.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,Anna Njoka amesema tatizo la udumavu lipo kwa 36% hasa kwa watoto wenye umri wa miezi 19-36,uzito pungugu 14.3% kwa wenye umri wa miezi zaidi ya 18 na ukondefu 6.6% kwa wale walio chini ya miezi 18.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,Iyogo Isuja amesema mkakati umewekwa wa kuanzisha kitalu cha miche ya zao la Parachichi ili isambazwe mashuleni kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi pamoja na kukuza mapato mashuleni.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.