Na Mwandishi Wetu
Serikali imekabidhi rasmi Shule mpya ya Msingi Kacheli kwa uongozi wa Kijiji cha Zeze, ikiwa na thamani ya Shilingi milioni 361. Shule hiyo itawahudumia wakazi wa vitongoji vya Lugufu Relini na Kacheli, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwapelekea wananchi elimu bora karibu na makazi yao.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo leo Alhamisi, Julai 24, 2025, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Paulo Ramadhani, amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika utunzaji wa miundombinu ya shule hiyo ili iweze kuhudumu kwa vizazi vijavyo.
“Miundombinu hii ina thamani kubwa. Kuna watu wasio na nia njema wanaoweza kuiba vifaa vya shule na kuhatarisha ubora wa majengo. Tunawaomba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzie ili kulinda rasilimali hizi za umma,” amesema Ramadhani.
Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa walimu watakaopangiwa kufundisha katika shule hiyo, hasa katika kutatua changamoto mbalimbali badala ya kila jambo kuachiwa Serikali pekee.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Ndelekwa Vanica, amesema ujenzi wa shule hiyo ulikamilika tangu Januari mwaka huu, na taratibu za kukabidhi rasmi kwa serikali ya kijiji zilikuwa zinaendelea ili kuwezesha wanafunzi kuanza masomo.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Zeze, Jonathan Ngongo, ameipongeza Halmashauri kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati kama ilivyoelekezwa kwenye mkataba wa ujenzi, huku akibainisha kuwa thamani halisi ya fedha imeonekana kupitia ubora wa majengo yaliyopo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.