Na Mwandishi Wetu
Nyachenda imeibuka kidedea kwenye Bonanza la Mpira kwa Vijiji Vinavyozunguka Hifadhi ya Shamba la Miti Makere baada ya kushinda mchezo wa fainali kwa goli 1-0 dhidi ya Makere pambano lililopigwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kitagata.
Akifunga mashindano hayo Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu amesema kuwa michezo inaimarisha afya pamoja mahusiano baina ya timu zinazoshindana.
“Michezo inaepusha ugomvi hivi ndio vitu tunavyovisema kwamba usalama wa eneo fulani au usalama wa nchi kiujumla unategemea sana kwenye michezo kwasababu tunapokuwa tunacheza tunakuwa tunaimarisha afya pamoja na usalama,” amesema.
Na kuongeza kuwa : “Tutumie michezo hii iliyodhaminiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambao mko nao karibu kwa kutunza mazingira ambayo wenzetu ndio wanayaifadhi kwakuwa yakiwa bora yanawafanya watu kuishi salama,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Emmanuel Ladislaus aliwapongeza TFS kwa ubunifu walioufanya kwa kuzikutanisha timu ambazo vijiji vyao vinazunguka hifadhi yao na kuoneshana uwezo hadi mshindi kupatikana.
Kocha wa Timu ya Nyachenda, Andrew Edward amesema siri ya mafanikio ni baaada ya kuwapa wachezaji wake maelekezo ya kutokaa na mpira ili ufike mbele kwa haraka kwa lengo la kuwachanganya wapinzani na kupelekea kufanya makosa.
Timu zilizoshiriki mashindano hayo ni Kagerankanda, Nyachenda, Nyakitonto, Mgombe, Makere, Kitagata, Kalimungoma, Chekenya, Mkiheta, Nyenge na TFS All Stars.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.