Na Mwandishi Wetu
Mfumo wa Kidigitali wa Uthibiti Ubora wa Shule (SQAS) unatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa utendaji kazi mashuleni, kwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Afisa Uthibiti Ubora wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Clement Mahanga, wakati wa mafunzo ya mfumo huo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kagoma, makao makuu ya halmashauri. Mafunzo hayo yamehusisha wathibiti ubora wa ndani ya shule pamoja na wakuu wa shule za sekondari.
“SQAS ni nyenzo muhimu inayowezesha shule kujiweka katika viwango halisi vya hali iliyopo. Hii inaimarisha utoaji wa taarifa kati ya shule na Ofisi ya Uthibiti Ubora,” alisema Mahanga.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo, Iyogo Isuja, alieleza kuwa mfumo huo pia utasaidia kuongeza uwajibikaji miongoni mwa watendaji wa elimu, pamoja na kuwezesha tathmini kufanyika kwa haraka na ufanisi zaidi.
“Hii ni hatua muhimu katika kuboresha elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia,” alisema Isuja.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Gumbo John, aliunga mkono matumizi ya mfumo huo, akisema kuwa tathmini za kidigitali zitasaidia kuleta mabadiliko chanya katika usimamizi wa elimu. Alitoa wito kwa shule zote kutumia mfumo huo kikamilifu ili kufikia malengo ya halmashauri ya kutoa elimu bora.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.