Na Mwandishi Wetu
Viongozi wa kada ya afya wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameagizwa kufanya usafi wa kina katika vituo vyao vya kazi siku ya leo Jumamosi shughuli itakayochukuliwa kama uzinduzi kuelekea kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu alipoongoza kikao kazi cha watumishi viongozi wa kada ya afya wilayani humo.
“Nitakapokuta watu wanafanya usafi hata wakiwa wawili nitaungana nao na kutamka uzinduzi rasmi kuelekea kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano nataka niwakute watu wapo ‘field’ hivyo sisemi nitakwenda wapi,” amesema.
Na kuongeza kuwa : “ Leo (jana) kazi hii nimeifanya Buhigwe wameanza kwa kupanda miti bahati nzuri tumepata wafadhili kutoka Jeshi la Uhamiaji ambalo limetoa miti 700 inayojumuisha 500 ya kivuli na 200 ya matunda,”.
Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele amewata watumishi wa kada ya afya kutumia ushawishi waliokuwa nao katika jamii kuwatoa watu upofu wa kujihusisha na masuala ya ramli chonganishi maarufu kama Kamchape au Lambalamba.
“Pale Shunguliba mwenzetu amepata madhara ameathirika kisaikolojia na kusababisha idadi ya wagonjwa kwenda pale kupungua hii hatutaki itokee maeneo mengine mwezio akipata tatizo mtie moyo na si kuanza kumdhiaki,” amebainisha.
Naye mwakilishi wa Jeshi la Zimamoto Konstebo, Chrisropher Moses ameshauri maeneo ya kutolea huduma za afya kuwa na vifaa vya awali vya kuzimia moto kwakuwa vinakuwa kama huduma ya kwanza sehemu ambayo dharura ya moto ikijitokeza.
Kwa upande wake Katibu wa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mphubusa Toyi amesistiza suala la kuwajengea uwezo watumishi wachanga wanaosimamia vituo vya afya ili wafanye kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Katika hatua nyingine Afisa Afya wa Halmshauri ya Kasulu Mji,Malimi Ntemisemi amesema kuwa sehemu zinazotoa huduma za afya zinatakiwa kuwa na vyoo bora vinavyokuwa katika hali ya usafi muda wote.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.