Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) Wilaya ya Kasulu chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Kamati hiyo ilifanya ziara siku ya jana kukagua utekelezaji ujenzi wa miradi ya maendeleo katika Shule ya Msingi Kalela ,Shule za Sekondari Kamuganza, kabagwe na Nkundusi pamoja na mradi wa maji wa Rusesa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwakisu amebainisha kuwa ameridhishwa na namna mafundi wanaotekeleza ujenzi wa miradi hiyo wanavyoifanya kwa weledi kitu kinachompa imani kuwa itakamilika vizuri.
“Lipo tatizo moja la watendaji wetu kuwa na masuala mengi ya michakato badala ya kutenda kazi na kusababisha ucheleweshwaji wa vifaa kwakuwa tunaitekeleza kupitia ‘Force Account’ hivyo lazima wachangamke ili miradi iweze kukaa sawa,” amesema.
Aidha, amesisitiza wananchi kushirikishwa katika kuchangia masuala mbalimbali ya maendeleo kwakuwa kuna mazingira mengine serikali inashindwa kukamilisha kila kitu.
“Kuna mazingira mengine serikali inashindwa kukamilisha kila kitu ni wajibu wetu kuchangia ili tuweze kuisaidia serikali kwenye baadhi ya mambo na mimi ndio mtu pekee ninayeweza kuidhinisha kitu chochote wazazi wanachoweza kuchangia,” amebainisha.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele amesema kuwa kumekuwa na utaratibu wa kukagua miradi zaidi ya mara moja kwa mwezi, kuangazia namna ya kuiboresha na kuikamilisha kwa wakati ili iweze kuleta tija katika jamii kama serikali ilivyokusudia.
“Niwaombe wasimamizi wa miradi wasisubiri ‘materials’ ziishe ndio waanze mchakato wa manunuzi, mifumo ya serikali ina utaratibu wake wakienda kwa wakati kwakujiongeza inasaidia upatikanaji wa vifaa kwa wakati,” amebainisha.
Katika hatua nyingine Theresia amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi mingi ya maendeleo katika wilaya hiyo hasa kwenye Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.