Na Mwandishi Wetu
Kilimo cha zao la mchikichi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kimeanza kuleta mafanikio makubwa kiuchumi kwa wakulima, kufuatia usambazaji wa bure wa mbegu bora aina ya Tenera. Hatua hii imechochea mageuzi makubwa kutoka kilimo cha mazoea kwenda kilimo cha kibiashara, jambo linalotarajiwa kuongeza tija, kipato, na ustawi wa wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika Kijiji cha Kiungwe, Kata ya Kitanga, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Masumbuko Kelemwa, amesema usambazaji wa mbegu hizo umefanyika kwa mujibu wa maelekezo ya serikali bila gharama yoyote kwa wakulima.
“Wakulima wetu wamehamasika kulima zao hili. Kuna mashamba si tu hapa Kiungwe, bali pia katika maeneo kama Rusesa, Bugaga na kata nyingine mbalimbali. Mbegu hizi tunazisambaza bure kabisa. tulianza na hekari 20, baadaye zikazidi kufikia 55, na sasa jumla ya wakulima 2,443 wamepata mbegu hizo na eneo la kilimo limefikia hekta 1,406 huku miche iliyosambazwa ikifikia 175,650,” amesema Kelemwa.
Ameongeza kuwa matarajio ya mavuno ni zaidi ya tani 300,000 kwa mwaka, huku halmashauri ikitarajia kunufaika kupitia ushuru wa mazao yatakayotengenezwa, kwani mazao hayo yanatarajiwa kuuzwaa ndani na nje ya nchi.
_
Mmoja wa wakulima wa zao hilo, Sadoki Mugama, ameishukuru serikali kupitia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mbegu hizo, ambazo huchukua muda mfupi kuanza kuzaa. Ambapo anategemea katika awamu ya kwanza ya mavuno kupata tani moja ya zao hilo, ambayo ni sawa na lita 100,000 za mafuta.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kiungwe, Enock Mugama, amesema kuwa kuna mapinduzi makubwa ya ulimaji wa zao hilo katika kijiji chake kutokana na upatikanaji wa mbegu bora pamoja na mafunzo ya kilimo waliyopewa wakulima bure, jambo ambalo limewafanya wakulima kuwa na matumaini makubwa ya kuboresha maisha yao.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.