Na Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imejiridhisha kuwa mchakato wa ombi la kuligawa Jimbo la Kasulu Vijijini umefuata taratibu zote za kikanuni kama inavyotakiwa na sheria na kanuni za uchaguzi.
Akizungumza jana Jumatano Aprili 23, 2025 katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kagoma, makao makuu ya halmashauri ya wilaya, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa INEC, Hamza Madali, amesema kuwa ombi hilo limewasilishwa kikamilifu kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria.
“Kikao hiki haina maana kwamba ombi lenu limekubaliwa, bali hapa tume imetimiza matakwa ya sheria ya 18 za kanuni ya INEC ya mwaka 2024 ya kutembelea majimbo yanayotaka kugawanywa au kubadilishiwa majina,” amesema Madali.
Ameongeza kuwa baada ya kikao hicho, tume itafanya uchambuzi wa kina wa taarifa zote zilizopokelewa na kufanya maamuzi ya mwisho kwa kuzingatia Ibara ya 75(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa INEC, Mtibora Selemani, amebainisha kuwa tume hiyo ilikuja kujiridhisha na hatua zote zilizochukuliwa katika mchakato huo, kuanzia ngazi ya halmashauri hadi mkoa, ikiwa ni pamoja na usahihi wa majina mapya ya majimbo yaliyopendekezwa — Buyonga na Makere.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Michael Ngayalina, akiongea katika tukio hilo amesema kuwa mchakato wa maombi hayo walihakikisha kwenye uandaaji wake unafuata taratibu zote zinazotakiwa kisheria.
Kwa upande wa wananchi, Diwani wa Kata ya Nyamnyusi, Mhe. Nathanael Ndelema, amesema kuwa jamii imehusishwa kikamilifu na taarifa zilizotolewa kwenye barua ya maombi ni sahihi, hivyo tume iendelee mbele na mchakato huo kwa niaba ya wananchi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.