Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, CPA Francis Kafuku, amewapongeza watumishi wa halmashauri hiyo kwa utendaji wao kazi bora na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii huku wakitembea kifua mbele kwa mafanikio waliyoonyesha.
Akizungumza leo Jumatano Julai 30,2025 katika kikao chake cha kwanza na watumishi wa makao makuu ya halmashauri pamoja na wale wa maeneo jirani, CPA Kafuku ameeleza kufurahishwa na hali ya kazi aliyoikuta wilayani humo, ikiwemo ukusanyaji wa mapato uliofikia 114% pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
“Nimefurahishwa sana na kazi yenu. Mmeonyesha weledi mkubwa kwa kukusanya mapato kwa kiwango cha juu na kukamilisha miradi kwa wakati. Mimi nikisema nimekuta hakuna kilichofanyika nitakuwa mwongo. Ombi langu ni moja tu: endeleeni kufanya kazi kwa bidii zaidi,” amesema.
Katika hatua nyingine, CPA Kafuku amewahimiza watumishi hao kuchangamkia fursa zilizopo wilayani Kasulu, hasa katika sekta ya kilimo na upandaji miti, ili kuongeza kipato chao binafsi.
“Kasulu ni eneo lenye fursa nyingi. Ningependa kuwaona watumishi wakijiongezea kipato kupitia kilimo na upandaji miti. Cha kushangaza, mtu anaajiriwa leo baada ya miezi mitatu tayari anataka kuhama. Unajuaje kama huku si pazuri? Ukiwekeza kwenye miti, mara nyingi huhitaji uangalizi mkubwa baada ya kupanda,” ameeleza kwa msisitizo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.