Wajumbe wa jumuiya za serikali za mitaa ALAT mkoa wa Kigoma, wametoa pongezi kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Joseph Kashushura kutokana na kazi nzuri anayoifanya kusimamia matumizi ya pesa za serikali na zinazotokana na mapato ya ndani katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo.
Pongezi hizo wamezitoa mwishoni mwa wiki walipokuwa katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Kigoma Jackson Mateso amesema, kinachofanywa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kinapaswa kuigwa na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Kigoma.
Kutolewa kwa kauli hiyo, kumetokana na taarifa iliyosomwa kwenye ziara hiyo ikionesha kuwa, halmashauri ya wilaya ya Kasulu imetumia zaidi ya shilingi milioni mia mbili kutokana na pesa za mapato ya ndani kujenga nyumba tano za watumishi wa idara ya afya.
"Sasa hapa kila mkurugenzi anaona, wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa wa Kigoma mnaona, tunaposema kuwa pesa zinazotokana na makusanyo ya ndani zinaweza kufanya kitu kikafanikiwa mfano wake tunauona hapa, hongera sana Mkurugenzi kwa maono yako na maono hayo yaendelee", amesema Mateso.
Pamoja na kutembelea ujenzi wa nyumba tano za watumishi, miradi mingine iliyofikiwa na ugeni huo ni ujenzi wa jengo la makao makuu ya halmashauri na wodi tatu za wagonjwa zinazoendelea kujengwa katika hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Kasulu.
Ziara hiyo ilifuatiwa na kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Akizungumza wakati wa kuahirisha kikao hicho, Mateso amewataka wajumbe wa kikao hicho kuzitumia ziara wanazozifanya kuwa na manufaa kwa kubadilishana mawazo, uzoefu na kudumisha mshikamano.
Mateso ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uvinza, amewataka wajumbe wa ALAT mkoa wa Kigoma kushiriki kikamilifu katika kufanikisha sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.