Zoezi la kuweka namba katika nyumba na majengo linaloendelea nchini, limeshika kasi katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma likichagizwa na ugeni wa viongozi kutoka mkoani na kwenye Wizara husika, anaripoti .
Wakizungumza wakati wa kikao cha mafunzo elekezi kwa makarani watakaokusanya taarifa za anuani za makazi kwenye halmashauri hiyo, Robert Mwakyami kutoka idara ya utumishi katika wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari na Rodrick Maduhu mratibu wa anuani za makazi mkoa wa Kigoma walisema, zoezi la anuani za makazi ni zoezi muhimu linalofanyika nchini linalotakiwa kutekelezwa kwa wakati na kwa makini.
Mwakyami na Maduhu wanaotembelea halmashauri za mkoa wa Kigoma kukagua maendeleo ya utekelezaji wa zoezi hilo walisema, wamepita katika halmashauri mbalimbali na kukuta utekelezaji ukiwa kwenye hatua tofauti tofauti na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo sanjari na watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa.
Akizungumzia mafunzo hayo, mratibu wa anuani za makazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Abudius Lubatu alisema, mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku mbili, yatahusisha nadharia na vitendo.
"Mpaka sasa zoezi linakwenda vizuri, tuko katika hatua ya kuweka namba kwenye nyumba na majengo kazi ambayo inafanywa na watendaji wa vijiji", alisema.
Aliongeza kuwa, kufanyika kwa kazi hiyo kutawarahisishia makarani watakapokuwa wakienda kukusanya taarifa.
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu yenye kata 21, vijiji 61 na vitongoji 283, inakadiria kuifanya kazi ya ukusanyaji wa taarifa za anuani za makazi, kwa muda usiozidi siku 15.
Picha ya juu ni Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Jackson Jekonia alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya makarani wa anuani za makazi, kulia kwake ni Robert Mwakyami afisa utumishi Wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari makao makuu na kushoto kwake ni Rodrick Maduhu mratibu wa anuani za makazi, mkoa wa Kigoma.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.