Watumishi wa Halmashauri ya Mji na Wilaya Kasulu wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) alipokutana na kuzungumza nao leo katika Ukumbi wa Chuo cha ualimu Kasulu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu), Mhe. George H. Mkuchika (Mb)(Mwenye suti nyeusi) akifafanua jambo wakati alipokutana na kuongea na watumishi wilayani Kasulu.
Na. Andrew Mlama-Kasulu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amekutana na kuongea na watumishi wa Umma toka Idara na Vitengo mbalimbali katika halmashauri ya Mji na Wilaya Kasulu.
Mkuchika amekutana na kuongea na watumishi hao leo Tarehe 24.09.2018 katika Ukumbi wa chuo cha Ualimu Kasulu, ambapo amewapongeza watumishi hao kwa kazi nzuri wanazozifanya kisha kusikiliza kero zao na kutoa ushauri wa namna bora ya kuzitatua.
Amesema utumishi wa umma ni pamoja na matumizi bora ya taaluma, nidhamu, kuzingatia kanuni za utumishi ili kuwa mfano wa kuigwa katika jamii. Amewashauri watumishi washirikiane katika kufanya kazi na kuongeza nguvu kukusanya mapato ili serikali iweze kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amefafanua kuhusu zoezi la uhakiki wa vyeti, ambapo amesema kuwa suala hilo lilizingatia Sheria na kanuni za kiutumishi. Kwa wale walioondolewa na kuthibitika hawana dosari za kiutumishi walirejeshwa kazini na kulipwa stahiki zao zote.
“Waliodanganya kiwango cha elimu, kugushi vyeti na walioajiriwa baada ya tarehe 20.Mei 2004 wakiwa hawana sifa ya ufaulu ya Mtihani wa Kidato cha nne, waliondolewa kazini kwa kuwa walijipatia ajira kinyume na utaratibu wa Serikali”amesema Mkuchika.
Waziri Mkuchika amewataka Wakurugenzi kutozuia barua za maombi ya uhamisho wa watumishi waliotimiza vigezo, bali watoe maoni yao kisha waruhusu barua zifike kwa aliyeandikiwa. Aidha amewataka Wakurugenzi watumie sababu za kibinaadamu kuruhusu uhamisho wa mtumishi endapo sababu za msingi zitathibitika.
Ametoa Rai kwa watumishi walioajiriwa Kigoma kuamini kwamba, wameajiriwa ili kuwezesha Wananchi kupata huduma na isiwe ni sehemu ya kupatia ajira kisha kuwaacha wananchi bila huduma.
Wakati huo huo Waziri Mkuchika, amewaasa watumishi wanaohusika na ukusanyaji mapato,jeshi la Polisi, Wauguzii na Sehemu nyingine zinazotoa huduma kwa Umma, waache na kuepuka vitendo vya Rushwa. Amesisitiza wafanye kazi kwa uadilifu ili kutoa huduma yenye usawa kwa wananchi wote.
Waziri Mkuchika amehitimisha ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kutembelea Kata ya Kitagata ambapo amezungumza na walengwa wa TASAF na kukagua shughuli za maendeleo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa kutokana na mradi huo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.