Na Mwandishi Wetu.
Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuhakikisha wananchi wanawapeleka watoto wenye umri wa chini ya miaka nane kwenda kupata chanjo ya ugonjwa wa Polio.
Hayo yamebainishwa leo wilayani humo na Afisa Usafi na Udhibiti wa Taka wa halmashauri hiyo, Ndelekwa Vanica aliyemwakilisha Mkurugenzi, Joseph Kashushura katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo ya Polio.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeona umuhimu wa kuendesha zoezi hilo katika mikoa sita ya Kigoma, Mbeya, Rukwa, Katavi, Songwe na Kagera litakalochukua muda wa siku nne.
“Zoezi hili litafanyika kwa awamu mbili awamu ya kwanza tunaizindua leo hadi tarehe 24 na awamu ya pili itakuwa mwezi Novemba kwa kuwafikia watu majumbani, kwenye vituo vya afya na maeneo yote ambayo tumeona kuna mkusanyiko wa watu unaojumuisha watoto wadogo,” amesema.
Pia amebainisha kuwa wilaya ya Kasulu imelenga kutoa chanjo hiyo kwa watoto wapatao 176,547 na kuwataka viongozi hao kuhakikisha wanawachukulia hatua watu wote watakaotaka kukwamisha zoezi hilo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kampeni Ngazi ya Mkoa, Dr Godfrey Smart amesema kuwa zoezi hilo limefanyika katika mikoa hiyo baada ya mkoa jirani wa Katavi mtoto kubainika kuumwa ugonjwa huo.
Pia amebainisha kuwa mkoa wa Kigoma umepanga kuwachanja watoto wapatao 884,000 na chanjo hiyo ni salama kwa kuthibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya.
Naye mmoja wa wananchi walioudhuria tukio hilo, Amina Zekieli akizungumza na mwandishi wetu amesema kuwa amesukumwa kuleta watoto wake kuja kupata chanjo hiyo ili kuwakinga na ulemavu wa kudumu siku za mbeleni.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.