Na Mwandishi Wetu
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Wakili Emmanuel Ladislaus, mapema leo Agosti 4, 2025, amefungua rasmi mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye Oktoba mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Wakili Ladislaus ameeleza kuwa uteuzi wa wasimamizi hao umezingatia masharti ya kisheria chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, ambayo inaweka misingi ya uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika mchakato wa uchaguzi.
"Napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wa kushiriki mafunzo haya muhimu. Ushiriki wenu ni ishara ya dhamira ya dhati ya kutumikia taifa kwa haki na uaminifu. Kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), nawapongeza kwa kupata nafasi hii adhimu," amesema Wakili Ladislaus.
Katika hatua nyingine, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata walikula kiapo cha uaminifu, utiifu na uadilifu, wakiahidi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu na kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo mbalimbali yatakayokuwa yanatolewa na Tume ili kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa kwa kila mpiga kura.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wasimamizi hao kuelewa vizuri Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi, pamoja na namna ya kushughulikia changamoto zitakazojitokeza wakati wa uchaguzi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.