Katika hali inayoonesha kufurahishwa na matokeo ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Bombwe katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba uliofanyika Novemba mwaka huu, afisaelimu msingi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi ametoa motisha ya shilingi laki moja kwa walimu wa shule hiyo.
Tukio hilo limetokea shuleni hapo mapema wiki hii wakati wa kikao cha wazazi na walimu kilichohudhuriwa na afisaelimu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na maofisa wengine.
Akisoma taarifa ya shule hiyo, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bombwe Neberth Lilabhabha amebainisha kuwa, shule ya msingi Bombwe imekuwa ya kwanza kwenye matokeo ya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kati ya shule 77 za halmashauri ya Wilaya ya Kasulu zilizokuwa na watahiniwa wa mtihani huo.
Amesema kuwa shule hiyo yenye walimu 6 na wanafunzi 886, ilikuwa na watahiniwa 57 wa darasa hilo kati yao 21 ni wasichana na 36 ni wavulana na wote wamefaulu mtihani huo.
"Wanafunzi wote wamechaguliwa kwenda shule za Sekondari tumefaulisha kwa asilimia mia moja," alisema mwalimu mkuu alipokuwa akisoma taarifa hiyo.
Matokeo hayo ambayo hayajawahi kufikiwa na shule hiyo tangu ilipoanzishwa takribani miaka 39 iliyopita, yalimwinua afisaelimu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Bi, Elestina Chanafi na kuwaambia kuwa, atatoa motisha ya shilingi laki moja kwa walimu wa shule hiyo.
"Natoa pesa hizo mfukoni mwangu iwe motisha kwa kazi nzuri mliyoifanya, mtaamua wenyewe kama mtanunua mbuzi mjipongeze ama vyovyote ", alisema Chanafi na kuwapongeza pia wazazi na viongozi wa kijiji na wa kata hiyo.
"Kutokana na mafanikio haya nimewapenda watu wa shule hii hata kabla ya kuwajua na nikaona leo nije tuonane", aliongeza Chanafi wakati wa hotuba yake.
Kikao hicho kilichohudhuriwa pia na diwani wa kata ya Buhoro Mathias Sunzu, kilikuwa na mafanikio makubwa hasa baada ya wajumbe wa kikao hicho kukubali kuyaendeleza mambo mbalimbali yaliyochagiza kupatikana kwa mafanikio hayo.
Makubaliano ya kikao hicho ni pamoja na wazazi kuhudhuria katika vikao pindi wanapohitajika, kukabiliana utoro wa wanafunzi, kuwepo kwa kambi ya kujiandaa na mitihani, kuchangia chakula cha wanafunzi, kuchangia malipo ya walimu wa kujitolea sanjali na kufuatilia maendeleo ya watoto wao wawapo shuleni.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.