Na Mwandishi Wetu
Ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha uhakika wa chakula nchini, wakulima wamehimizwa kujisajili au kuhuisha taarifa zao kwa ajili ya kunufaika na mbolea ya ruzuku.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro, leo Ijumaa Agosti 8, 2025, wakati akifunga Maonesho ya Wakulima wa Kanda ya Magharibi yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Ipuli mkoani Tabora, yakihusisha mikoa ya Kigoma na Tabora.
“Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kukuza sekta ya kilimo kwa kutoa mbolea ya ruzuku, hususan kwa mazao ya chakula kama mahindi. Hivyo nawasihi wakulima kutumia mbegu bora kwani ubora wa mazao huanza na ubora wa mbegu. Ukipanda mbegu duni, usitarajie mavuno bora,” amesema Balozi Sirro.
Aidha, amezitaka taasisi za kifedha zinazotoa mikopo kwa wakulima kuhakikisha zinafanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha mikopo hiyo inatumika kama ilivyokusudiwa. Amesema hatua hiyo itasaidia kilimo kuwa cha tija na kuongeza uzalishaji.
Kwa upande mwingine, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa kanda hiyo, Vaileth Lusana ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira bora ya ulipaji kodi, jambo ambalo limeimarisha uhusiano kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Naye mwakilishi wa wakulima, Wallwa Makoye, ameiomba Serikali kuweka mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wasitegemee mvua pekee katika uzalishaji, hatua itakayowawezesha kulima kwa mzunguko wa mwaka mzima na kuongeza tija katika kilimo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.