Na.Andrew Mlama-Kasulu.
Wakazi wa Kata ya Makere iliyopo wilayani hapa, wameamua kuwasaidia wenzao walio kwenye kaya duni katika kuwajengea nyumba ili kuwapunguzia adha ya ukosefu wa makazi bora na kuwafanya wawe na afya bora, furaha na amani.
Akizungumza na mtandao wa www.kasuludc.go.tz, diwani wa viti maalum kata ya Makere Bi. Mwasi Mchunga, amesema mpango huo waliuanza baada ya kuanzisha zoezi la kukagua kaya zisizo na vyoo ambapo walibaini asilimia kubwa ya kaya zenye hali duni kiuchumi ndizo zisizo na vyoo. Kupitia vikao vya kamati ya maendeleo ya kata, waliunda kamati iliyochunguza na kubaini uhitaji mkubwa wa msaada ili kuhakikisha wakazi hao wanapata mahitaji muhimu sambamba na uwepo wa vyoo.
Msaada unaotolewa na wakazi hao ni ujenzi wa nyumba, vyoo bora, manunuzi ya vyombo vya ndani na malazi kwa makundi yenye uhitaji ikihusishwa wazee wa jinsia zote, walemavu, wajane wanawake wenye watoto ambao wametelekezwa na waume zao na kaya zilizo masikini.
Kupitia vikao vyake, kamati hiyo iliwashawishi na kuwahimiza wananchi wote kuona umuhimu wa kuchangia fedha na nguvu ili kuhakikisha wenzao wasiojiweza wanapata nyumba, vyoo malazi na mahitaji mengine muhimu, jambo ambalo wananchi kwa kauli moja waliafiki na kuanza utekelezaji kupitia viongozi waliopo katika vitongoji vyao kwa awamu mbalimbali.
“Wananchi wanapochangishwa au kutakiwa kuchangia nguvu, wamekuwa wakijisikia huru huchangia bila kusita na haupo mgogoro wowote uliokwisha jitokeza kutokana na uendeshwaji wa zoezi hilo katani hapa”amesema bi.Mchunga.
Amewahamasisha wanajamii wanaopenda maendeleo na kujali thamani ya utu wa wengine wilayani Kasulu na kwingineko kote nchini, waweze kufika Makere kwa ajili ya kujifunza utaratibu huo na wakaufanyie kazi pale wanapoishi kwani jamii zenye uhitaji zipo nchi nzima.Mbali ya kuwa ni utaratimu kusaidiana, hata imani za dini zetu zinatuhamasisha kufanya hivyo kwa wahitaji.
Amehitimisha kwa kusema kuwa, kwa sasa kata ya Makere wanaelekea kupunguza hali ya watu kutokuwa na vyoo bora kwani kaya nyingi zina vyoo bora na vya kisasa vyenye hadhi ya kutunza utu wa mtu pamoja na kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Aidha ujenzi wa idadi ya vyumba katika nyumba hizo huendana na idadi ya watu waliopo katika kaya husika kuendana na mahitaji halisi pia misaada mingine hutolewa kwa walengwa kuendana na kiwango cha fedha kinachokuwa kimekusanywa na ni utaratibu endelevu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.