Na Mwandishi Wetu
Lengo la Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kwa ngazi ya halmashauri ni kuibua vipaji vitakavyounda timu bora kwenye michezo mbalimbali ili ziweze kufanya vizuri katika ngazi ya mkoa.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Michezo na Sanaa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Thomas Kisaka ameyabainisha hayo jana wilayani humo katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Kasulu kwenye uzinduzi wa mashindano hayo kwa ngazi ya halmshauri.
“Michezo ya UMITASHUMTA ngazi ya halmashauri maana yake tunachukua watoto waliofanya vizuri kwa ngazi ya kata na kuwashindanisha ili tuweze kupata vipaji tutakavyoingia navyo kambini na kupata timu ya halamshauri itakayokwenda kushindana na halmshauri zingine nane ili kupata timu ya Mkoa wa Kigoma,” amesema.
Naye mmoja ya wajumbe anayehusika na suala la kuchagua washiriki , Stellah Ikanga amesema kuwa uwa wanangalia mchezaji ambaye hafanyi makosa sana pamoja na nafasi anayocheza ni namna gani anatimiza majukumu yake.
Na kuwataka wazazi kuwaruhusu watoto kushiriki michezo hiyo kwakuwa wanakuwa wapo katika uangalizi salama pamoja na kupata mahitaji yote muhimu yanayojumuisha malazi, chakula na matibabu iwapo tatizo likitokea.
Mwakilishi wa Benki ya NMB Wilaya ya Kasulu, Samwel Kabatemi amesema kuwa tofauti na msaada wa maji walioutoa kwa wanamichezo watahakikisha mipira inapatikana kwa haraka kama walivyoombwa na wasimamizi wa michezo hiyo.
“Tunafahamu michezo ni afya mimi niwasihi tu katika kipindi chote hiki cha michezo yenu tujali afya zetu ukiona mwili umechoka sana ni vizuri kuwasiliana na daktari kwakuwa michezo ni burudani,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Afisa Elimu Msingi (Taaluma) wa halmshauri hiyo, Joseph Maige ameishukuru Benki ya NMB kwa kuwa wadau wakubwa wanapofuatwa kutatua changamoto zao mbalimbali hasa katika sekta ya elimu.
“Naamini msaada walioutoa utakwenda kufanikisha lengo lililokusudiwa la mashindano haya kitu kitakachoboresha ufanisi wa wachezaji watakapokwenda kupambana na halamshauri zingine,” amebainisha.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.