Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Rusesa Ndg. Sadi Amri Sadi.
Muonekano wa Jengo la Nyumba ya Mganga katika Kituo cha Afya Rusesa likiwa katika hatua za ukamilishwaji.
Na. Andrew Mlama.-Kasulu Vijijini.
Ujenzi wa kituo cha Afya katika Kata ya Rusesa wilayani hapa, unaendelea vizuri na unaelekea kukamilika kutokana na utendaji kazi mzuri unaosimamiwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kushirikiana na watendaji wake kwa kutumia utaratibu wa “Force Account”.
Akizungumza na mtandao wa www.kasuludc.go.tz, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Ndg. Sadi Amri Sadi, amesema mradi huo unaogharimiwa na fedha kutoka Serikali kuu Jumla ya Shilingi Mil. 500, unahusisha ujenzi wa jengo la upasuaji, Wodi ya kina mama,Nyumba ya Mganga, jengo la kuhifadhia maiti na ujenzi umefikia katika hatua za ukamilishaji.
Amesema ujenzi huo wa miundo mbinu ya Afya unatarajiwa kukamilika hivi karibuni ambapo utasaidia kutatua changamoto za huduma kwa wagonjwa hususani uwepo wa wodi ya kisasa ya kujifungulia kwani jengo lililopo sasa halikidhi mahitaji.
“Ujenzi wa miundo mbinu ya Kituo hiki cha Afya ni muhimu sana kwani tunahudumia wagonjwa kutoka katika vijjiji mbalimbali vya Kata za Bugaga, Muzye, Kigembe, Rusesa, Kalela, Kwaga, na baadhi ya vijiji vilivyopo Halmahsauri ya Kigoma vijijini pamoja na Uvinza”amesisitiza Sadi.
Ameendelea kusisitiza kuwa mara baada ya majengo hayo kukamilika, Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri kuhakikisha vifaa kwa ajili ya upasuaji na huduma ya kwanza kutokana na dharura mbalimbali zinazojitokeza vinapelekwa mapema kituoni hapo. Utekelezaji wa huduma hizo za haraka umekuwa changamoto kituoni hapo ambapo uhitaji wake ni mkubwa.
Kahiyu Kaloli ambaye ni Afisa Muuguzi Msaidizi Kituoni hapo, ameiomba Serikali ihakikishe ujenzi wa miundo mbinu hiyo uende sambamba na ongezeko la watumishi hali itakayorahisisha utoaji huduma katika kituo hicho.
“Tuna changamoto kubwa ya utoaji wa huduma kutokana na wingi wa wagonjwa wanaotoka sehemu mbalimbali za wilaya ya Kasulu pamoja na wilaya za jirani”amesema Kaloli.
Ameuomba uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Idara inayohusika na Ajira pamoja na masuala ya kiutumishi , ione haja ya kuongeza watumishi kituoni hapo kutokana uwepo wa Ikama ndogo ya watumishi waliopo kituoni hapo hali inayopelekea kutotoa huduma kwa kadri ya matarajio.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.