Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Isaac Mwakisu ametoa wito kwa mashirika ya umma na sekta binafsi kuiga mfano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaotatua changamoto za miundombinu mashuleni wilayani humo.
Mwakisu ameyabainisha hayo jana kwenye makabidhiano ya madawati 50 yaliyotolewa na TSF katika Shule ya Msingi Nyanzanza iliyopo Kijiji cha Kagera Nkanda wilayani humo.
“Niombe taasisi zingine kuiga mfano wa TFS ambao wanajitoa sana mimi toka nimefika wamekuwa wanatoa kipaumbele kwa kile wanachokipata kukirudisha kwa jamii,” amesema.
Aidha, amewataka wakazi wa kijiji hicho kufanya kazi kwa karibu na TFS ili misitu wanayoitunza iendelee kuwepo kitu kitakachosaidia utoaji wa misaada zaidi yenye tija kwa jamii.
Pia, amewataka walimu wa shule hiyo kuhakikisha wanawaelekeza wanafunzi namna bora ya utunzaji wa miundombinu iliyopo shuleni hapo ikiwemo madawati ili iweze kutumika na vizazi vijavyo.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Buhigwe na Makere, Deograsian Kavishe amesema kuwa utoaji wa madawati hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 80 inayoelekeza uboreshaji wa mazingira ya kufundishia mashuleni.
“Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi tumetoa madawati haya ili kutengeneza mitaji watu hawa watoto mnaowaona hapa kila mtu ana karama yake lakini zisipoendelezwa zinaweza zisiibuke katika kutimiza ndoto zao,” amebainisha.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Issaya Salum ameishukuru TFS kwa misaada mbalimbali waliyotoa katika shule hiyo ikiwemo mifuko 100 ya Saruji, Gypsam bodi 60, tanki la maji la lita 500, upandaji wa miti 500 eneo la shule pamoja kutoa elimu ya upandaji miti na utunzaji wa misitu kwa walimu na wanafunzi.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele amesema kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kutekeleza mradi wa maji ili wananchi wa kijiji hicho huduma hiyo iweze kuwafikia.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.