Na Mwandishi Wetu
Mwalimu Yusufu Hamisi ‘U Fresh’ leo Jumatano Agosti 21,2024 ametoa bima za afya nane kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Buchuma iliyopo Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu kupitia shirika lisilo la kiserikali la Usilie Tena (UTO).
Akizungumza katika tukio hilo Yusufu ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi Kisuma amesema kuwa huwa anapambana kutafuta wadau ili watoto wenye mahitaji maalum wilayani humo waweze kufikiwa na huduma za afya kwa lengo la kuwapunguzia mzigo huo wazazi.
“Msaada huu wa matibabu tuliopewa na UTO utakuwa msaada mkubwa si tu kwa wazazi pia hata kwa walimu inawezekana mtoto amezidiwa akapelekwa hospitali mzazi ukafuata kuliko anazidiwa unapigiwa simu unaanza kutafuta hela ili aende kupata matibabu,” amesema.
Aidha, Yusufu amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Semistatus H. Mashimba kwa msisitizo ambao huwa anautoa kwa watumishi kujiongeza kwenye shughuli nyingine ambazo zitakuwa msaada kwa jamii.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buchuma, Rachael Mwamboja amekemea tabia ya baadhi ya watu kuwanyanyapaa watoto wenye mahitaji maalum kitu kinachopelekea wazazi kuwaficha majumbani hivyo kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Naye Mwalimu wa Takwimu wa Shule ya Msingi Buchuma, Karist Kanuti amesema kuwa shule hiyo ni jumuishi inayohusisha pia watoto ambao si walemavu hivyo huwa wanajitahidi suala la kusaidiana linakuwepo baina ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo, Edson Bukene amewataka wazazi walioudhuria tukio hilo kwenda kuwa mabalozi kwa wazazi wenye watoto kama hao kuwa wanaweza kupata elimu kama wengine pamoja na kupata misaada mbalimbali kutoka kwa wadau tofauti.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.