Na Mwandishi Wetu
Shule ya Sekondari Nyenge iliyopo Kata Kurugongo katika Halamshauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma mapema leo Mei 29, 2024 imepokea vitabu vya kiada kutoka kwa Mdau wa Elimu, Donald Lugelela vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kwa lengo la kuboresha masuala ya taaluma shuleni humo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Lugelela amesema kuwa vitabu hivyo vimefanikiwa kufika hapo kupitia Maktaba Kuu ya Tanzania na wadau kama yeye kuvipata kwa ajili ya kuvigawa katika taasisi na shule mbalimbali.
“Vitabu nilivyoleta vinatolewa na Shirika la Book Aid International la nchini Uingereza kupitia Maktaba Kuu ya Tanzania ndio sisi wadau tunavileta kwenye taasisi na shule mbalimbali haviji hapa nchini moja kwa moja vinapitia katika taasisi zinazoeleweka na serikali na vinachambuliwa kabla ya kuanza kusambazwa,” amesema.
Afisa Elimu Sekondari (Taaluma) Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mussa Kanyoe amebainisha kuwa si jambo dogo kwa mtu aliyezaliwa eneo fulani kukumbuka nyumbani kwao na kuleta msaada mkubwa kama huo wenye mashiko utakaosaidia vizazi vingi.
“Shule hii ilianza kujengwa na wananchi wa Nyenge ilipofikia hatua ya Lenta serikali ikachukua mradi tumshukuru sana Mhe. Rais . Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuona wazazi wa nyenge wamejitoa akaingiza mkono wake kusaidia jitihada zao na wewe leo (Lugelela) umeunga juhudi zake mkono kwa vitendo,” amesema.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Akibar Sanga amemshukuru mdau huyo kwa kuunga juhudi za Mhe. Rais . Dkt. Samia Suluhu Hassan anayetilia mkazo suala la watoto wa kitanzania kupata elimu ili waweze kutimiza ndoto zao.
“Binafsi nimshukuru mdau kwa kutuletea vitabu ambavyo vitaongezea watoto wetu maarifa kwasababu ni vitabu vya ziada baada ya kupata vitabu ambavo vimeteuliwa kwa ajili ya ufundishaji wataweza kuongeza maarifa zaidi,” amebainisha.
Katika hatua nyingine Kaka Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyenge,Deus Chokero amesema vitabu hivyo vitawasaidia katika kujisomea kwakuwa vimeweka maarifa kwa upana zaidi kitu kinachompa imani katika ufanyaji wao wa mitihani watapata alama nzuri na hivyo kutoa ujinga kwenye taifa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.