Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mha. Godfrey Kasekenya (aliyesimama)akielezea jambo wakati wa ufunguzi mafunzo Elekezi kwa watumishi wa Idara ya Afya (hawapo pichani). Kulia kwake ni Afisa Utumishi Charles Millinga. (wa kwanza kushoto) Dk. Robert Rwebangira Kaimu Mganga Mkuu wilaya, akifuatiwa na Afisa Tawala Ndg. Nicholaus na watatu ni Katibu wa Afya Ndg. Joseph Mwanambesi.
Watumishi wa Idara ya Afya wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu(hayupo pichani) wakati wa Ufunguzi wa mafunzo Elekezi kwa watumishi walioajiriwa kuanzia Mwaka 2017, Waganga wakuu wa Vituo vya Afya na Zahanati yaliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka wakuu wa vituo vya Afya na Zahanati kufanya kazi kwa kushirikiana na watumishi walio chini yao ili kupata matokeo makubwa ya utendaji kazi ambayo ni tija kwa halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo tarehe 7.1.2019 alipokuwa akifungua Mafunzo elekezi kwa Watumishi wa Idara ya Afya walioajiriwa kuanzia mwaka 2017, Waganga wakuu wa Zahanati na vituo vya Afya yaliyolenga kuwakumbusha Sheria na Maadili ya utumishi wa Umma, usimamizi wa fedha, na taratibu za kiutendaji kwa Kada ya Afya wilayani hapa.
“Ukiwa kiongozi wa Kituo cha Afya au Zahanati, ukaunda timu ya kufanya kazi na mkashirikiana vizuri na watumishi walio chini yenu kwa kuzingatia umoja, upendo,ushirikiano na mkafanya kazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, lazima mtapata matokeo makubwa na mazuri” amesema Kasekenya.
Amewasisitiza watumishi hao kuhakikisha wanasimamia matumizi ya Fedha zinazoelekezwa vituoni kwa kuzingatia miongozo, kudhibiti upotevu wa dawa, kuweka ulinzi kwenye Zahanati na vituo vya Afya, kujiendeleza kitaalumana na kutulia vituoni kwani maeneo mengi ya wilaya ya kasulu yanafikika na yana huduma nyingi muhimu.
Kaimu Mganga Mkuu Wilaya, Dk.Robert Rwebangira amesema Mafunzo na maelekezo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi hao katika utendaji kazi wenye Weledi na kuwasaidia maelekezo na ushauri utakaowapa mwanga katika utatuzi wa changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kiutendaji kazi.
“Pia kupitia mafunzo haya, watafahamu na kutekeleza dhana ya ugatuzi wa madaraka toka Halmashauri mpaka kwenye vituo vya Afya na Zahanati”amesisitiza Rwebangira.
Ndg. Joseph Mwanambesi ambaye ni Katibu wa Afya Wilaya, amesema kuwa, kupitia mafunzo hayo anatarajia watumishi husika watatoa huduma bora kwa wananchi na kufanya kazi kwa kuzingatia Kanuni na taratibu za kiutumishi hali itakayoondoa migogoro isiyo ya lazima baina yao na waajiri hali kadhalika wananchi wanaowahudumia.
Upande wake Bi. Vailet Raymond ambaye ni Afisa Tabibu wa Kituo cha Afya Nyenge, amesema mafunzo hayo yamesababisha atambue masuala mbalimbali ikiwemo Sheria za kiutumishi, miundo ya vyeo, taratibu na kanuni za utendaji kazi.
“Binafsi niseme mafunzo haya yamenipa mwanga na kupelekea kujitambua nafasi yangu kama mtumishi wa Umma na ninajisikia kuanza utendaji kazi upya” amesisitiza Vaileth.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.