Imeelezwa kuwa serikali inaendelea kufanyia kazi suala la utoaji wa mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kutengeneza utaratibu mzuri utakaokuwa na ufanisi.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Mobutu Malima kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya wazazi ambayo kimkoa yamefanyika kwenye Kata ya Nyakitonto wilayani Kasulu.
“Serikali ilisitisha mikopo hii baada ya kuona wakinamama ndio walikuwa warejeshaji wakubwa tofauti na makundi mengine hivyo inapanga utaratibu mwingine wa kudhibiti hali hii,” amesema.
Na kuongeza kuwa : “ Halmashauri zote nchini zimekuwa zinaendelea kutenga fedha na fedha zipo muda wowote utaratibu ukitoka ni namna gani mikopo itolewe fursa zitatangazwa na wananchi wote wajitokeze,”.
Aidha, Malima amesema kuwa serikali haijalala katika kupambana na wapiga ramli chonganishi maarufu kama Kamchape na wale wote watakaohusika na vitendo hivyo wakifikishwa katika vyombo vya sheria itakuwa ni halali yao.
Naye Mwenyeti wa CCM Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe amewaonya makada wa chama hicho kujiepusha na masuala ya Kamchape kwakuwa yanadhalilisha watu.
“Ukikamatwa na wewe ni kiongozi wa CCM na unashiriki vitendo hivyo vya kitapeli usikanyage katika ofisi za CCM kwasababu tutakuchukulia na wewe ni sehemu ya tatizo nenda katumike huko,” amebainisha.
Awali akizungumza katika sherehe hizo Mwenyekiti wa Wazazi CCM Wilaya ya Kasulu, Selema Wandwi amewataka vijana kuchangamkia fursa kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.