Na Mwandishi Wetu
Serikali imekuwa inaongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo pamoja na ile ya Mifugo na Uvuvi ili kuimarisha masuala ya ugani na miundombinu ikiwa na lengo la kuwezesha ukuaji wa sekta hizo muhimu zinazogusa maisha ya watanzania wengi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha amebainisha hayo jana wakati akifunga maonesho ya Nanenane Kanda ya Magharibi yaliyokuwa yanaendelea mkoani humo.
Amesema kupitia ongezeko hilo la bajeti serikali iliandaa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ili kuwavutia vijana kuwekeza katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi na kuhakikisha soko linakuwepo kwa kile kitakachozalishwa.
“Kupitia BBT serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kujenga kesho iliyo bora kwa kuwapa mafunzo ya kufanya kilimo kilicho bora kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu na mbinu mbalimbali za kufanya kilimo na ufugaji wenye tija,” amebainisha.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye amesema kuwa umuhimu wa sekta ya mifugo na ufugaji unajieleza wazi kwakuwa ni nyenzo muhimu kwenye kujitosheleza kwa chakula hivyo uzalishaji wake kuwa na uhakika wa soko.
Na kuongeza kuwa juhudi za dhati zinatakiwa kufanywa kwenye sekta za kilimo,mifugo na uvuvi ili kusaidia uzalishaji wa kutosha wa malighafi kwa ajili ya uchakataji viwandani kitu kitakachosaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yanayotokana na sekta hizo.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Eliasifu Mlai aliwahimiza wakulima kutumia teknolojia sahihi katika kilimo wanachokifanya ikiwemo matumizi ya mbegu bora ili kiwango cha uzalishaji wa mazao kipate kuongezeka.
Katika hatua nyingine Mwakilishi wa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Magharibi,Mathias Zacharia amewataka wakulima kujiunga na Bima ya Mazao ili wawe na uhakika wa usalama wa kile wanachokizalisha mashambani.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.