Mkazi wa Kasulu Aziz Rajab, akiwa chini ya uangalizi wa Tabibu Jasmen Meru wakati akijitolea damu kwenye maadhimisho ya uzinduzi wa Kampeni ya Jiongeze tuwavushe salama iliyozinduliwa leo Tarehe 13.3.2019 Mjini Kaulu.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange akitambulisha wageni mbalimbali waliohudhuria kwenye uzinduai wa kampeni ya Jiongeze! tuwavushe salama iliyofanyika kwenye uwanja wa umoja Mjini Kasulu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brig. Mstaafu Emmanuel Maganga akihutubia wakazi wa Mji wa Kasulu(hawapo pichani) waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni ya Jiongeze! Tuwavushe salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mha. Godfrey Kasekenya (Mwenye Miwani) akiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Kamati ya Ulinzi, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Jiongeze! Tuwavushe salama iliyofanyika Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Mku wa Mkoa wa Kigoma Brig. Mstaafu Emmanuel Maganga akikabidhi Mkataba pamoja na vipeperushi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mha. Godfrey Kasekenya. Utaratibu huo ni katika kuhakikisha utekelezaji wa kampeni hiyo unafanyika na Halmashauri zitoe kipaumbele katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.
Wasanii wa Bendi ya Kasulu Theatre Group(KATAG) Wakishusha Burudani ya nguvu kwa wageni na Wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Jiongeze! katika Uwanja wa Umoja mjini hapa.
Na. Andrew Mlama.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brig. Mstaafu Emmanuel Maganga amezindua Kampeni ya kitaifa Mkoa wa Kigoma “Jiongeze! Tuwavushe salama” yenye lengo la kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga nchini Tanzania.
Uzinduzi wa kampeni hiyo yenye madhumuni ya kuhamasisha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za Afya Familia na wanajamii kwa ujumla ili kuchangia juhudi za Taifa za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga, umefanyika leo tarehe 13.2.2019 katika uwanja wa Umoja uliopo mjini Kasulu.
Brigedia Mstaafu Maganga mesema kuwa, tendo la uzazi sio adhabu ya Kifo kwa mama bali ni agizo la Mungu tuzaane. “Wazazi wote ni lazima washirikiane na wataalam wa Afya kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa Salama” amesema Maganga.
Amesisitiza wakina mama kupaza sauti zao ili waweze kwenda Kliniki na wazazi wenzao kwa lengo la kupokea na kufanyia kazi Elimu na ushauri wa Wataalam wa Afya kwa pamoja ili kuhakikisha usalama wakati wa uzazi na malezi bora ya mtoto atakayezaliwa.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameshuhudia wakuu wa wilaya 8 za Mkoa wa Kigoma wakitia Saini makubaliano yatakayozitaka halmashauri hizo kutoa kipaumbele katika masuala ya uzazi na watoto.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa, lengo la uzinduzi wa Kampeni hiyo liwe chachu kwenye kuongeza nguvu na msukumo katika kuhakikkisha mama na mtoto hawapotezi uhai kwa sababu ya uzazi.
Katika Risala yake kwa Mgeni Rasmi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dk. Paul Chaote, ametoa takwimu za wastani wa vifo vitokanavyo na vizazi kitaifa na kimkoa. Kwa mujibu wa tafiti za kitaifa kwa mwaka 2015/2016, wastani wa vifo vya uzazi 556 katika vizazi 100,000 hupoteza Maisha ambapo lengo ni kupunguza hadi kufikia 212 kwa 100,000 ifikapo 2020.
Upande wa watoto wachanga, wastani wa vifo kitaifa unaonesha watoto 25 hufariki kati ya vizazi hai 1000 ambapo lengo ni kupunguza hadi kufikia vifo 16 katika vizazi hai 1000 kwa mwaka 2020.
Kwa Mkoa wa Kigoma mwaka 2016 takwimu zinaonesha vifo 97 sawa na vifo 148 kwa vizazi 100,000, Mwaka 2017 vifo135 , 2018 vifo 77 kwa vivazi 100,000. Kwa watoto wachanga vifo vimeendelea kupungua toka watoto 18 kati ya 100,000 hadi vifo 8 kwa mwaka 2018.
DK. Chaote amezitaja sababu za vifo hivyo ikiwa ni kuvuja Damu nyingi, Kifafa cha Mimba, upungufu wa damu na uambukizo baada ya uzazi. Aidha ametoa takwimu za Idadi ya kina mama wanaojifungua kwenye vituo vya Afya zikionesha mwaka 2016 waliojifungua ni 63.6%, 2017 ikiwa 78.5% na 2018 ikiwa 98.5%.
Amewasisitiza wakina mama wanapopata ujauzito kuanza kuhudhuria kwenye vituo vya Afya wakiwa katika hatua za awali badala ya kusubiri baada ya Miezi mitatu hadi mitano. “Utaratibu huo utatoa fursa kwa matabibu kubaini hali hatarishi inayoweza kujitokeza mapema na kukabiliana nazo hali itakayopelekea uzazi salama’’ amesisitiza Dk. Chaote.
Kilele cha uzinduzi wa Kampeni ya Jiongoze! Tuwavushe salama, kimefikiwa ambapo Mgeni Rasmi Brigedia Mstaafu. Emmanuel Maganga amekata utepe na kukabidhi vipeperushi na Mikataba ya usimamaizi na uendeshaji wa Kampeni hiyo kwa wakurugenzi wa Miji na Wilaya za Mkoa wa Kigoma.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.