Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, ameagiza ujenzi wa mabanda ya kudumu katika Viwanja vya Nanenane Ipuli, mkoani Tabora, kwa washiriki wa kudumu zikiwemo halmashauri, taasisi za umma, na sekta binafsi.
Lengo la hatua hiyo ni kupunguza gharama za maandalizi kila mwaka kwa taasisi hizo maonesho hayo pindi yanapokaribia.
Mhe. Chacha ametoa maelekezo hayo leo Ijumaa, Agosti 2, 2025, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Nanenane Kanda ya Magharibi, yanayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma.
Ameeleza kuwa ujenzi wa mabanda hayo ya kudumu utasaidia kuweka miundombinu bora itakayowawezesha wananchi kupata elimu ya kitaalamu kuhusu fursa na teknolojia mbalimbali katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha, Mhe. Chacha amewahimiza wakulima kuhakikisha wanashiriki kikamilifu mpango wa mbolea ya ruzuku kwa kujisajili au kuhuisha taarifa zao, ili waweze kunufaika na punguzo hilo. Vilevile, amewataka wafanyabiashara wa mbolea kufuata bei elekezi iliyowekwa na Serikali ili kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo hizo kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Twalib Njohole, amesema kuwa lengo la maonesho hayo ni kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza teknolojia bora zitakazoongeza tija katika uzalishaji.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kwari Bura, amesema kuwa wizara hiyo inaendelea na kampeni ya kutoa chanjo kwa mifugo dhidi ya magonjwa manne ambayo ni homa ya mapafu kwa ng’ombe, mdondo kwa kuku, kideli, na mafua ya kuku.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.