Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya akifafanua jambo mara baada ya kuwasilisha taarifa ya ujenzi wa Kituo cha biashara mjini Kasulu. Kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Ndg. Rashid Mchanga na wa tatu kushoto ni Naibu katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Bw. Tixon Tuliangine Nzunda.
Naibu katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Bw. Tixon Tuliangine Nzunda akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhia maji taka katika Jengo linalokamilishwa la Kituo cha Biashara kilichopo Mjini Kasulu.
Jengo la kituo cha Biashara “One Stop Business Centre lililopo Mjini Kasulu.
Na. Andrew Mlama-Kasulu.
Naibu katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Bw. Tixon Tuliangine Nzunda amekagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Biashara cha Wilaya “One Stop Business Centre” kilichopo kata ya Kimobwa Mjini Kasulu.
Nzunda amekagua kituo hicho leo tarehe 12.11.2018 akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa kuboresha Mazingira ya Biashara(Local Investment Climate-LIC) mkoani Kigoma. Mradi huo wa kituo cha Biashara “One Stop Business Centre” umetekelezwa na LIC ikishirikiana na Halmashauri ya mji na wilaya ya Kasulu ambapo umegharimu shilingi. 49,977,177.61.
Amesisitiza watendaji kuhakikisha wanatekeleza maelekezo yote wanayoyapata ili kufikia malengo yaliyowekwa na yanayoendelea kuwekwa na Serikali. Aidha amesema, hatoweza kumfumbia macho mtu yeyote atakayebainika kuzorotesha shughuli za maendeleo kwa namna yoyote.
“Nimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hiki na ninakuagiza Mkuu wa Wilaya uhakikishe kinafunguliwa na kuanza kutumikahivi karibuni” amesema Nzunda baada kumaliza kukagua Kituo hicho.
Akiwasilisha taarifa ya miradi iliyotekelezwa na inayotegemewa kutekelezwa na LIC, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema mpaka sasa kituo kipo kwenye hatua za mwisho za ujenzi na mafundi wanakamilisha mfumo wa maji safi na maji taka pamoja na kuunganisha Umeme.
Amesema wanaotarajiwa kutoa huduma katika jengo hilo ni pamoja na maafisa biashara wa halmashauri za mji na wilaya ya Kasulu, Afisa toka mamlaka ya mapato, huduma za kibenki, TCCIA pamoja na BRELA.
Amefafanua kuwa, mpaka sasa vimeshapokelewa vifaa mbalimbali kutoka LIC ambavyo ni Kompyuta sita, Printa moja, meza sita, Kabati sita,Viti vya Ofisini kumi na nane pamoja na viti sita vya wageni.
“Tunatarajia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja wetu na kuimarisha mahusiano na taasisi mbalimbali” amehitimisha Kasekenya.
Nzunda ameendelea na ziara yake ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Mradi wa kuboresha mazingira ya biashara (LIC) mkoani hapa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.