Na Mwandishi Wetu
Shirika la World Vision kupitia mradi wa Buhoma kwa kutumia mtindo wa Mtazamo Chanya limekuwa linatoa mafunzo kwa jamii ili kuiwezesha kufunguka kiakili na kiuwezo iweze kuona fursa mbalimbali zinazowazunguka na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuwaletea maendeleo.
Hayo yamebainishwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma hivi karibuni na Mwezeshaji wa Mradi huo, Zablon Choma kwenye kikao cha kufanya tathimini kwa wanufaika wa mradi ni jinsi gani mafunzo waliyopata yameweza kuinufaisha jamii inayowazunguka.
Amesema mradi huo unafanya kazi kwenye Tarafa ya Makere yenye kata nane na vijiji 10 kwa kushirikiana na serikali ili kutatua changamoto zinazoikabili jamii katika eneo hilo.
“Mwaka jana kwa kushirikiana na viongozi wa serikali tulipata wawakilishi 12 kutoka vijiji 10 na kuwajengea uwezo na baada ya kuwafundisha wakarudi katika vijiji vyao kwenda kufanya mambo mbalimbali katika sekta ya kilimo, ufugaji na biashara,” amebainisha.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Evaristo Milagrokasase amesema kupitia mafunzo hayo amepata uelewa kuwa mtu akitaka kufanikiwa si lazima aende mbali bali awe na uwezo wa kuzitumia kikamilifu fursa zinazomzunguka katika eneo lake la karibu.
“Awali nilikuwa nalima kilimo cha kawaida lakini mwaka uliopita nilipata kujua Pamba ni dhahabu nyeupe hivyo mwaka huu nina mpango wa kulima heka mbili na mahindi tayari nimelima heka saba, na kupata pongezi nyingi kwa namna ninavyoendesha kilimo changu,” amebainisha.
Mnufaika mwingine Emelisiana Manyurane amebainisha kuwa kupitia shughuli za ufugaji alizoanza kuzifanya baada ya mafunzo amefanikiwa kusomesha watoto wake wanne na mjukuu mmoja, kujenga nyumba pamoja na kununua kiwanja chenye thamani ya shilingi milioni 1.2.
Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Kitagata, Eliud Mteze amesema kuwa jukumu lake katika mradi huo ni kuwaelimisha wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake wahamie katika mtindo ule wa biashara.
“Kwa kutambua hilo nimeanza na vikundi vinavyojihusisha na shughuli hizi kwa kutoa huduma za ushauri bure na pale ninapokutana na mapungufu najitahidi kuwaelimisha ili wafanye kilimo pamoja na ufugaji wenye tija,” amesema.
Akifunga kikao hicho Afisa Maendeleo ya Jamii, Jotham Daniel amesema ufuatiliaji wa yale yote yaliyozungumzwa utaanza kufanyika hivi karibunii ili kujiridhisha uhalisia wake kama ni kweli.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.