Na Mwandishi Wetu
Muongozo mpya wa utoaji wa mikopo ya 10% kwa makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu umeelekeza Menejimenti ya Halmashauri kuwa sehemu ya kamati kwa kuhusika na kuidhinisha utoaje wake kwa vikundi vilivyokidhi vigezo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,Ndelekwa Vanica wakati wa mafunzo ya wakuu wa divisheni na vitengo kuhusiana na mikopo hiyo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kagoma uliopo makao makuu ya halmshauri.
“Maelekezo tuliyopewa ni kwamba menejimenti ni sehemu ya kamati kwahiyo usishangae siku muhandisi au mtu wa kilimo ukaulizwa hali ya mikopo huko kwenu inaendaje uwe na majibu yanayoeleweka ndio maana tumeitana hapa leo,” amesema.
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Victoria Makyao amesema kuwa kwenye kundi la walemavu watazingatia ule ambao unaonekana kwa macho na mwenye uwezo wa kufanya shughuli za kumuingizia kipato.
Naye Mratibu wa Mikopo hiyo,Pelimina Msuta amebainisha kuwa ili kikundi kipate mkopo ni lazima wanachama wake wawe raia wa Tanzania,kwa kundi la vijana umri kuanzia miaka 18 hadi 45,wanaofanya shughuli za uzalishaji mali, leseni ya biashara,idadi ya watu watano na kuendelea na kuwa na akaunti ya benki.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Halmashauri hiyo, George Msonge amesema kuwa wajibu wa Menejimenti ni kupokea na kujadili mapendekezo ya mikopo kutoka Kamati ya Huduma ya Mikopo ya Halmshauri ili iweze kupitishwa au kukataliwa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.