Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa jana Agosti 13,2024 amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na kufanya mkutano wa adhara na wananchi wa Kata ya Kagera Nkanda ambapo kupitia mkutano huo ametoa maelekezo yafuatayo;
Ameupa muda wa wiki mbili Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini Tanzania (TARURA) mkoani humo kufanya tathimini na mapitio kuangalia ni namna gani barabara ya kilomita 18 inayokwenda katika kata hiyo invyoweza kufanyiwa ukarabati ili iweze kupitika vipindi vyote vya mwaka.
Pia, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya kwa kushirikiana na wataalam wa afya kutoka TAMISEMI kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika kata hiyo.
“Mkurugenzi wa Afya TAMISEMI na Katibu Mkuu mwakilishi wa Katibu Mkuu ninawaelekeza anzeni mchakato wa kutenga fedha pamoja na halmshauri kutenga fedha na sisi TAMISEMI lazima tutenge fedha ili kuwasaidida wananchi wa Kagera Nkanda waweze kupata Kituo cha Afya,” amesema.
Aidha, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kasulu pamoja na viongozi wote wa wilaya hiyo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili waweze kujiunga na mfumo wa Bima ya Afya ulioboreshwa (CHF) ambao mchango wake ni shilingi 30,000 kwa mwaka inayojumuisha idadi ya watu sita ili wananchi waweze kupata matibabu bila shida.
Vilevile, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini kuhakikisha wanalinda haki za watanzania kwa kuangalia haki ya mtu mmoja isivuke mipaka ya haki ya mtu mwingine kwakuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kila siku uwa anasisitiza jambo hilo.
Katika hatua nyingine Mchengerwa ametoa hakikisho kwa wakazi wa kata hiyo kuwa wataalam wa TAMISEMI watafika hapo hivi karibuni kuja kukagua eneo itakapojengwa shule ya kidato cha tano na sita, na taarifa hiyo itakapomfikia mezani mchakato wake utaanza mara moja baada ya kupitiwa na kuthibitishwa na wananchi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.