Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Emmanuel Ladislaus, amesema mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya uandikishaji wakati wote wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili, ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi na weledi.
_
Akizungumza leo Jumanne Aprili 29, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uboreshaji wa Daftari hilo katika Chuo cha Ualimu Kasulu, Ladislaus ameeleza kuwa ingawa mawakala hao wataruhusiwa kuwa vituoni, hawataruhusiwa kuingilia majukumu ya maafisa waandikishaji.
“Ni muhimu mawakala wawe na mipaka ya utekelezaji wa kazi zao ili kuepusha mwingiliano usio wa lazima na kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufanisi,” amesema Ladislaus.
Katika hatua nyingine, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanatunza vifaa vyote vitakavyokuwa katika vituo vya uandikishaji na kufuata kwa makini maelekezo yatakayotolewa na Afisa Mwandikishaji.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamesema yamewajengea uwezo mkubwa wa kiutendaji. Yasinta Kasunzu amesema mafunzo hayo yatamsaidia kusimamia vyema waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki katika kituo chake.
_
Naye Essau Hinyura ameeleza kuwa mafunzo hayo yameongeza weledi wake katika kusimamia shughuli za uandikishaji, huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi pindi awamu ya pili ya zoezi hilo itakapoanza, ili waweze kupata haki ya kushiriki uchaguzi kama inavyotakiwa na Katiba.
_
Zoezi la uandikishaji na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili linatarajiwa kuanza Mei 1 hadi 7, 2025. Wananchi wote wenye sifa wanahimizwa kujitokeza kwa ajili ya kujiandikisha au kuhakiki taarifa zao.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.