Makarani wa sensa ya watu na makazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma waliokuwa wakifanyia mafunzo yao kwenye chuo cha ualimu Kasulu, wamehamishia mafunzo hayo katika vijiji vya Makere, Nyakitonto, Kasangezi na Rungwe mpya.
Mabadiliko ya mahali pa kufanyia mafunzo hayo yanatokana na takwa la mwongozo wa sensa ya watu na makazi wa mwaka 2022 kuhusu kufanyika kwa mazoezi ya kudodosa ambapo kwa makarani wa halmashauri za vijijini wanatakiwa kufanya mazoezi hayo kwa kuhoji kaya zilizo katika maeneo ya vijijini kama ilivyo kwa makarani wa halmashauri za mijini wanaotakiwa kufanyia mazoezi hayo kwa kuhoji kaya za mjini.
Akizungumza muda mfupi kabla ya makarani hao kuanza safari ya kwenda vijijini, mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu aliyefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mafunzo hayo, amewaasa makarani hao kuvitunza vishikwambi walivyokabidhiwa kwa ajili ya kazi hiyo na kujiepusha na ulevi muda wote watakapokuwa kwenye kazi hiyo.
"Kavitunzeni vishikwambi hivyo kama mboni za macho yenu maana hivyo ndio vitendea kazi vyenu, na mimi nawaombea kwa mungu mtakapokuwa huko, pepo la ulevi lishindwe na mkaifanye kazi hiyo kwa mafanikio makubwa", alisema.
Kufuatia mabadiliko hayo, zaidi ya makarani 1300 waliokuwa kwenye mafunzo hayo kituo cha chuo cha Ualimu Kasulu, wameondoka kuelekea vijijini wakiambatana na wakufunzi wao.
Watakapokuwa huko, sambamba na kufanya mazoezi kwa vitendo, makarani hao pia watafundishwa jinsi ya kujaza dodoso la jamii na dodoso la majengo madodoso ambayo yamepangwa kufundishwa wakati wa mazoezi hayo.
Mafunzo hayo yaliyoanza Julai 31, yanatarajiwa kufikia kikomo Agosti 19 siku chache kabla ya kuanza kwa zoezi la kuhesabu watu.
Pichani makarani wakimsikiliza mkuu wa Wilaya ya Kasulu alipofika kuzungumza nao.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.