Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu Ndg. Nimrod Kiporoza akifungua mafunzo ya Awali ya Mipango na Bajeti ya masuala ya lishe ngazi ya Halmahsauri yaliyofanyika leo Tarehe 23.11.2019 kwenye ukumbi wa Halmashauri wilayani hapa.Kulia kwake ni Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Dk. Robert Rwebangra na Kushoto ni Afisa Afya (w) Ngd. Ngaraba.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mafunzo ya awali ya Mipango na Bajeti kutoka Halmashauri ya Mji na wilaya ya Kasulu.
Na.Andrew Mlama-Kasulu DC.
Mafunzo ya awali ya Mipango na Bajeti kwa ajili ya masuala ya lishe Ngazi ya Wilaya, yamefanyika wilayani hapa ambapo wawezeshaji wa kitaifa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Afisa Afya Mkoa na Maafisa lishe wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Kasulu wametoa mafunzo na Takwimu mbalimbali za hali ya Lishe kwa baadhi ya Wataalam wa Afya na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri hizo mbili.
Akifungua Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika leo tarehe 23.11.2018, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kasulu Ng. Nimrod Kiporoza, amesema lishe ni kichocheo cha Maendeleo ya Elimu, Kilimo, Biashara,Afya, Uchumi na ustawi wa Jamii kwa ujumla. Uboreshaji wa masuala ya lishe na kudhibiti utapiamlo utapelekea jamii kumudu kufikia malengo ya maendeleo kwa urahisi. Amefafanua kwamba, makundi athiriwa na utapiamlo ni Wanawake walio katika umri wa kuzaa ambao ni kati ya miaka 15 hadi 49 na watoto wadogo wenye umri wa miezi O hadi miaka 5. Kiwango cha udumavu utokanao na utapiamlo mkoani Kigoma ni 37.9%, kiwango ambacho ni zaidi ya Kile cha kitaifa cha 34%.
Ameendelea kueleza kuwa, mpaka sasa Halmashauri ya Kasulu imesha andaa Kamati za lishe ngazi zote na maafisa lishe waliopo wanaendelea na majukumu yao. Hii ni katika kutekeleza mpango jumuishi wa utekelezaji Afua za Lishe nchini wa Julai 2015/2016 hadi Juni 2010/2021 uliozinduliwa Dodoma na Mh. Kasim Majaliwa(MB) Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Nawaagiza kila mtu kwa nafasi yake, mfuatilie kwa umakini na udadisi mkubwa na mkayatumie mafunzo haya kuboresha hali za lishe kwa watoto na kina mama ili kufikia malengo ya kitaifa. Serikali ya Awamu ya tano inatambua umuhimu wa lishe kwa ustawi wa Taifa ili kufikia Uchumi wa kati wa Maendeleo ya viwanda ifikapo mwaka 2015. Twende na tukumbuke lishe bora ni msingi wa Maendeleo kwa Taifa letu” Amehitimisha Kiporoza.
Akiwasilisha mada, Mwezeshaji kitaifa Ndg. Apolinary Andrew amefafanua kwamba sababu zinazosababisha utapiamlo na kupelekea hali ya udumavu ni pamoja na lishe duni au isiyozingatiwa, wazazi kutokujali malezi bora ya watoto, hali ya Afya za watoto na kina mama na kutozingatia utaratibu mzuri wa unyonyeshaji watoto.“Lishe bora ni muhimu kwa mtoto kuanzia ujauzito mpaka anapotimiza miaka miwili ambapo jumla yake ni siku elfu moja za malezi ili kumjengea makuzi mazuri ya kiakili na kimwili” amesema Andrew.
Upande wake Kaimu Afisa lishe Mkoa Bi. Naomi Rumenyela, amesema lengo la mafunzo ni kupata uelewa juu ya masuala ya lishe ili wanamafunzo wakayatumie kueleimisha jamii umuhimu na athari zitokanazo na kutozingatia lishe bora. “Mtoto mwerevu anaweza kupatikana iwapo wazazi na walezi tutazingatia masuala ya lishe kwa umakini” . Ametoa msisitizo Bi. Naomi.
Mchangia mada, Baraka Godson ambaye ni Mwanasheria wa Halmashauri ya mji Kasulu , amesema masoko ya usiku yamekua changamoto kubwa katika masuala ya lishe. Akina mama hurudi nyumbani usiku sana na kukuta watoto mamelala hali inayopelekea watoto wengi kulala bila kula mlo wa usiku. amesema elimu lishe ikifika kwa usahihi itaweza kuwasaidia kina mama kujua athari zitokanazo na watoto kushindwa kupata mlo kwa wakati.
Akichangia mada, Afisa Utumishi na Utawala wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Ngd. Kiwoli, amesema Mila na Desturi zimechangia jamii nyingi kukabiliwa na tatizo la lishe duni kwa watoto na kina mama. “Jamii nyingi zimekuwa zikimtazama zaidi baba katika kuhakikisha anapata chakula kizuri na cha kutosha wakati watoto na kina mama hubaki wakila mlo usio katika ubora au usio tosheleza” amesisitiza Kiwoli.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Robert Rwebangira, amewasisitiza wana mafunzo kuhakikisha kila Idara na Kitengo kwa nafasi yao wanahakikisha wanabeba jukumu la kutoa Elimu ya lishe wanapopata nafasi ya kukutana na wana jamii wakiwa katika mazingira yao utekelezaji wa majukumu ya kila siku. kwa kufanya hivyo watasaidia kukabiliana na tatizo la lishe linalopelekea udumavu utakaoathiri Jamii na kupunguza kasi ya utendaji kazi na maendeleo kwa ujumla.
Washiriki wa mafunzo hayo, wamepewa maelekezo ya namna ya kupangia mipango na bajeti ya utekelezaji wa masuala ya lishe katika Halmashauri zao kwa kutumia mfumo wa PlanRep. Aidha wameshirki kujadiliana mbinu mbalimbali za kupata fedha zitakazotumika kuhakikiksha mkakati wa Elimu ya lishe na unatekelezeka wake unafanyika ili kuhakikisha malengo ya kitaifa yanafikiwa kwa ufasaha.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.