Na Mwandishi Wetu
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu leo Jumatano Machi 12,2025 limeridhia pendekezo la kuanzishwa jimbo jipya ambapo mchakato wake ukikamilika katika ngazi za juu kutakuwa na majimbo mawili ya Makere na Buyonga.
Ambapo kupitia maazimio hayo kutakuwa na ongezeko la Kata tano za Kabulanzwili, Nyenge na Nyakafyeke zitakazokuwa Jimbo la Buyonga huku zile za Kitema na Mnarani zitahusika na Jimbo la Makere.
Akizungumza katika Mkutano Maalum wa Baraza hilo uliofanyika katika Ukumbi wa Kagoma uliopo Makao Makuu ya Halmashauri Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Laurent Poteza amesema kuwa maazimio hayo yatasaidia kuimarisha uwakilishi wa wananchi katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Mhe. Agustino Vuma Holle amebainisha kuwa iwapo azma yao itafanikiwa itasaidia kupunguza mzigo wa kiutawala,kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na ugawaji wa bajeti kwa ufanisi tofauti na sasa kutokana na jimbo hilo kuwa na eneo kubwa la kiutawala.
Awali akizungumza katika tukio hilo Afisa Uchaguzi wa Halmshauri hiyo, Komesha Kaminyoge amesema kuwa baada ya menejimenti kuchunguza na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau imeona kuna haja ya kuwasilisha mambo hayo katika mkutano huo maalum.
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ni moja kati ya mbili zilizopo ndani ya Wilaya ya Kasulu ikiwa na jimbo moja la Kasulu vijijini,Tarafa Nne, Kata 21, Vijiji 61 na vitongoji 283 huku likiwa na Kilomita za mraba 7,081.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.