Na Mwandishi Wetu
Maafisa Waandikishaji wasaidizi Ngazi ya Kata wametakiwa kuongeza umakini katika utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwani kwa kutofanya hivyo kutapelekea athari kubwa katika ukamilisaji wa zoezi hilo muhimu.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kasulu Vijiji, Emmanuel Ladislaus alipokuwa akifunga mafunzo ya Uboreshaji wa Daftari La Kudumu la Wapiga Kura jana Julai 14, 2024.
Na kuwataka maafisa hao kulitekeleza zoezi hilo kwa weledi ikiwemo kuzingatia muda wa kufungua na kufunga vituo vya wapiga kura.
Aidha, amesisitiza kuzingatia matumizi mazuri ya lugha kwa wananchi wanapofika katika vituo hivyo kwani kwa kufanya hivyo itakua ni hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uandikishaji na kusaidia kazi kufanyika kwa unadhifu na haki.
“Nendeni mkafanye kazi kwa busara na hekima hakikisheni mnakuwa na matumizi ya lugha nzuri katika utekelezaji wa majukumu yenu huku mkifuata maelekezo na miongozo yote ya tume ili kazi yenu ifanyike kwa haki na unadhifu”,amesema Ladislaus.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Amos Madaha amewataka Maafisa hao kuhakikisha wanazingatia muda kwani katika kuhakikisha zoezi hilo halikwami.
“Kama mnavyofahamu zoezi hili linaenda na ratiba vituo vifunguliwe kwa muda maalum na kufungwa katika wakati maalumu ili Halmashauri yetu iendelee kuwa mfano mzuri kati ya halmashauri 8 zilizopo katika Mkoa wa Kigoma”, amesema Madaha.
Zoezi la Uboreshaji la Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kufunguliwa Kitaifa kwa awamu ya kwanza katika mkoa wa Kigoma, na zoezi hilo litafanyika katika mkoani humo pamoja na mikoa ya Tabora na Katavi kuanzia tarehe Julai 20-26, 2024.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.